• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Sh100m: Wabunge wa Kenya ndio wengi zaidi duniani kwa kongamano Amerika

Sh100m: Wabunge wa Kenya ndio wengi zaidi duniani kwa kongamano Amerika

LUCAS BARASA na CHARLES WASONGA

WAANDALIZI wa kongamano la wabunge nchini Amerika wamefichua orodha ya watu 85 ya ujumbe wa Kenya katika mkutano huo.

Ujumbe wa Kenya ndio mkubwa zaidi kati ya mataifa mengine ya dunia.

Pia imebainika kuwa ujumbe huo wa wabunge, maseneta na madiwani ulijumuisha wafanyakazi 22 wa bunge ambao majukumu yao katika kongamano hilo hayakujulikana.

Ujumbe huo unaoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka unakadiriwa kutumia zaidi ya Sh100 milioni, katika safari hiyo ambayo imekosolewa na Wakenya wengi akiwemo kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Mnamo Jumatano, wabunge walipinga ripoti iliyochapishwa katika gazeti la Daily Nation kuhusu uwakilishi wa Kenya katika kongamano hilo wakidai ilipotosha.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi Aden Duale, wabunge hao walilipa gazeti hilo makataa ya siku saba liombe msamaha la sivyo walishtaki mahakamani.

Mkutano huo ambao ulikamilika Alhamisi, ulifanyika katika mji wa Nashville katika jimbo la Tennessee.

Wengine waliohudhuria ni kiongozi wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen, mwenzake wa wachache James Orengo na seneta wa Kakamega Cleophas Malala.

Vile vile walikuwemo maseneta Susan Kihika (Nakuru), Aaron Cheruiyot (Kericho), Ali Abdullah(Mteule), Beth Mugo (Mteule), Mutula Kilonzo Jr (Makueni), Falhadfa Iman (Mteule), George Khaniri (Vihiga) na Okong’o O’ Mogeni (Nyamira).

Bunge la kitaifa liliwakilishwa na wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Cecily Mbarire (Mteule), Omboko Milemba (Emuhaya), Julius Mawathe (Embakasi Kusini), Ben Momanyi (Bonchari), Bi Tecla Tum(Nandi), Daniel Tuitoek (Mogotio) kati ya wengine.

Makamishna wa Tume za Huduma za Bunge (PSC), Samuel Chepkonga, Aisha Jumwa, Naomi Shabaan na Bi Lonah Mumelo pia wako katika orodha ya ujumbe kutoka Kenya.

Mabunge ya kaunti yaliwakilishwa na maspika John Kaguchia (Nyeri), George Ndoto (Kitui), madiwani 14 kutoka mabunge mbalimbali na maafisa watatu wa mabunge hayo.

You can share this post!

Sossion apata fursa ya kuponda Magoha kwenye kizaazaa

Komeni kutegemea misaada na kuwa walafi, Amerika yaikemea...

adminleo