Waandamanaji wapinga mauaji ya raia nchini DRC
Na AFP
WAANDAMANAJI wapatao 5,000 waliziba barabara na kuteketeza magurudumu katika mji wa Beni mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kulalamikia msururu wa mauaji katika eneo hilo, polisi walisema.
Kufikia Ijumaa, watu sita walikuwa wameuawa ndani ya muda wa saa 24 na watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa makundi ya wapiganaji. Raia wengine wengi wameripotiwa kutoroka makwao kufuatia mashambulio hayo.
“Waandamanaji hao pia waliziba barabara kuu za kuingia katikati mwa jiji hali ambayo iliwapa maafisa wa usalama kibarua kigumu cha kuzizibua kwa kuiondoa miamba na magurudumu yaliyotumika,” akasema kamanda wa polisi Kanali Safari Kazingufu.
Bw Kizito Bin Hangi ambaye ni mkazi wa jijini la Beni alisema wakazi, haswa vijana, waliamua kufanya maandamano kwa kurusha mawe barabarani na kuteketeza magurudumu kwa kuchukizwa na ongezeko la visa vya mauaji ya watu kiholela.
“Kwa hakika sio jambo zuri, mauaji yanatokea kila siku,” akasema Hinga ambaye ni afisa wa shirika la kijamii eneo hilo.
“Hii ndio maana vijana waliamua kufanya maandamano na kuwahimiza wakazi wengine kususia kazi zao,” akaongeza.
Maaandamano sawa na hayo yalifanyika jijini Beni Jumatano huku raia wakitembea kwa zaidi ya kilomita 15 hadi katika afisi ya Kikosi cha Umoja wa Mataifa (UN) cha kulinda amani, kuwasilisha barua ya malalamishi.
Makundi kadha ya wapiganaji hufanya mashambulio katika eneo la Beni lililoko mkoa wa Kivu Kaskazini, yaking’ang’ania kudhibiti utajiri wa madini.
Moja ya makundi hayo ni lile la Allied Democratic Forces (ADF) ambalo limetuhumiwa kuwaua mamia ya raia katika miaka ya hivi karibuni.
Sita wauawa kijijini Mbau
Katika shambulio la hivi punde watu sita waliuawa katika kijiji cha Mbau na wapiganaji wa kundi kisichojulikana. Jeshi la DRC lilithibitisha mauaji ya watu hao
“Adui aliwasili ghafla usiku mwendo wa saa mbili na nusu usiku. Watu sita waliuawa wakitoroka. Niliona maiti za wanaume watano na mwanamke mmoja. Wanne waliuawa kwa risasi na wawili kwa panga,” Noella Katongerwaki, rais wa mashiriki ya kijamii katika eneo la Beni aliambia AFP.
Lakini wanawake wawili na watoto wawili bado hawajulikani waliko, akaongeza.
Vilevile, watu watano walitekwa nyara katika kijiji cha Mayele, Bi Katangerwaki aliongeza.
Kando na mauaji yanayosababishwa na makundi ya wapiganaji, eneo la Beni pia limeshuhudia vifo kutokana maradhi hatari ya Ebola ambayo imeua jumla ya watu 1,800 nchini DRC tangu mwaka 2018.