Habari Mseto

Nyoro adai jopo la BBI ni njama ya kumfaa Raila tu

August 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na NDUNGU GACHANE

MBUNGE wa Kiharu Ndindi Nyoro, amepuuzilia mbali juhudi za Jopo la Maridhiano (BBI) kubadili Katiba, akisema kuwa lengo lake kuu ni kupitisha kauli ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhusu uongozi wa nchi.

Bw Nyoro alidai kuwa ripoti ambayo itaandikwa na jopo hilo imetolewa na Bw Odinga, akisema kuwa ndiye kiongozi wa pekee anayelielewa hilo kwa undani.

Alisema kuwa azma yake ni kulitumia kuendeleza malengo yake ya kisiasa.

Kulingana na Bw Nyoro, Bw Odinga anapinga Mswada wa Punguza Mizigo, unaoendeshwa na Dkt Ekuru Aukot wa chama cha Thirdway Alliance ili kutoa nafasi kwa ripoti ya BBI.

Alisema kuwa jopo hilo limependekeza kuandaliwa kwa kura ya maoni, kama anavyotaka yeye Bw Odinga.

“Kwangu binafsi, mchakato mzima wa kusikiliza maoni ni kupitisha mipango ya Bw Odinga. Ni yeye pekee anayefahamu shughuli za jopo hilo kwa undani. Hiyo ndiyo sababu kuu anapinga mswada wa Dkt Aukot, kwani anaamini mipango yake ndiyo sahihi kila wakati,” akasema.

Alidai kwamba jopo hilo liliamua wale ambao walifika mbele yake ili kutoa maoni na walielekezwa vile wangewasilisha mapendekezo yao.

Alisema kuwa matokeo ya ripoti yake yaliamuliwa kitambo ili kutoa nafasi ya maandalizi ya kura hiyo ya maoni.

Alidai jopo hilo tayari lina ripoti yake ya mwisho, inayopendekeza kubuniwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu ili kumtengenezea nafasi Bw Odinga kurejea katika uongozi wa nchi.

“Rais Uhuru Keyatta amenukuliwa akisema kuwa haungi mkono kura ya maamuzi lakini ripoti ya BBI itapendekeza maandalizi yake ili kubadilisha mfumo wa utawala, kauli ambayo Bw Odinga amekuwa akiiunga mkono,” akadai Bw Nyoro.

Kwa upande wake, mbunge wa Kandara Alice Wahome alisema kuwa jopo hilo halina msingi wowote wa kisheria.

Alilitaja kama kundi la kisiasa ambapo lengo lake kuu ni kusambaratisha azma ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais katika mwaka wa 2022.

Alisema kuwa jopo hilo lilifanya vikao vyake kwa kutumia pesa za mlipa-ushuru.

“Watu hawajui vile kundi hilo lilibuniwa, kwani umma haukuhusishwa. Viongozi, vilevile, hawafahamu undani wa sababu ya kubuniwa kwake. Ni kundi tu ambalo lengo lake ni kuzima mipango yote ya kisiasa ya Dkt Ruto,” akasema.

Jopo lawekwa gazetini

Jopo hilo lenye wanachama 12 liliwekwa kwenye gazeti rasmi la serikali Mei 2018 na linaongozwa na Seneta Yusuf Haji wa Garissa.

Limezuru kaunti zote 47 kukusanya maoni ya wananchi kuhusu masuala ambayo yamekuwa yakizua migawanyiko nchini, hasa uchaguzi.

Jopo hilo lilimaliza vikao vyake mnamo Ijumaa baada ya kupokea maoni kutoka kwa viongozi wa Kiislamu, ambao walikuwa kundi la mwisho kuwasilisha maoni.

Kwa sasa, linaandaa ripoti yake ambayo litawasilisha kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga kabla ya mwisho wa mwezi Septemba.

Hata hivyo, wanachama wake wamekuwa wakipinga kauli kuwa lengo lake ni la kisiasa.