• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Jumwa apata pigo akimpigia debe mwaniaji wa udiwani

Jumwa apata pigo akimpigia debe mwaniaji wa udiwani

Na CHARLES LWANGA

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa amepata pigo kisiasa baada ya wagombeaji watatu wa chama cha ODM kuungana kumpigia debe mmoja wao kama mgombeaji mkuu katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda, Kaunti ya Kilifi.

Uchaguzi huo mdogo umepangwa kufanyika Oktoba 17.

Bi Jumwa ambaye alikosana na chama chake cha ODM kwa kupigia debe azimio la Naibu Rais William Ruto kugombea urais mwaka wa 2022, alikuwa ametangaza kuwa atamuunga mkono Bw Abdulrahaman Omar, ambaye pia ameasi ODM ili kuwania udiwani kama mgombeaji huru.

Kiti hicho cha Ganda kilibaki wazi baada ya Mahakama ya Rufaa mjini Malindi kukubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu kuwa uchaguzi wa Bw Omar uliofanywa Agosti 8, 2017 haukuwa wa huru na haki, na ikaamuru uchaguzi urudiwe tena.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa wamedai kuwa uchaguzi mdogo wa Ganda utakuwa mtihani wa ubabe kati ya Bi Jumwa na magavana Hassan Joho (Mombasa) na mwenzake Amason Kingi (Kilifi)pamoja na kubainisha umaarufu wa ODM eneo hilo.

Mabw Joho na Kingi ndio wanatambuliwa kushikilia usukani wa ODM katika maeneo ya Pwani.

Lakini, baadhi ya viongozi wa ODM eneo la Malindi pamoja na wafuasi na madiwani walimtangaza mgombeaji wa chama atakuwa Bw Rueben Katana, ambaye aliwania kwa chama cha Kadu Asili.

Uwaniaji wa Bw Katana ambaye alimshtaki Bw Omar na Tume ya Uchaguzi (IEBC) na kushinda kesi iliyofanya uchaguzi urudiwe, umepigwa jeki na wagombeaji mwenza-Bw Ibrahim Kaniki na Bw Erastus Juma, baada ya kukubaliana.

Mkataba huo ambao uliandikwa na kupigwa sahihi na kunakiliwa kwa mwenyekiti wa chama, Bw Amason Kingi na ODM, ilishuhudiwa na madiwani Nixon Muramba (Kakuyuni), Bw David Kadenge (Malindi Town) na Bw Gilbert Peru wa Sokoni.

Wakizungumza na wanahabari baada ya kuweka mkataba, madiwani hao watatu walimuonya Bi Jumwa dhidi ya kuingilia siasa za chama cha ODM wanapojitayarisha kuelekea uchaguzi mdogo wa Ganda.

“Baadhi ya viongozi ambao walichaguliwa kwa chama cha ODM akiwemo Bi Jumwa wameasi chama wakidai wamejiunga na timu sishuki na viuno, tunataka tuwaambie wawachane na siasa za Ganda,” alisema.

Alisema kutokana na demokrasia na umoja wa chama cha ODM, wagombeaji hao walikubaliana kumpigia debe mgombeaji mmoja mkuu badala ya kushiriki kura ya mchujo.

Bw Kadenge alikanusha madai kuwa chama cha ODM kimeisha nguvu na kupoteza umaarufu eneo hilo akisema wako tayari kushinda uchaguzi wa Ganda.

“Baadhi ya viongozi wamekuwa wakieneza propaganda kuwa ODM imepoteza umaarufu lakini nataka kuwaambia kuwa Malindi bado ni ngome ya ODM, waliotuwacha watuwache na amani kwa sababu tulikupenda lakini Mungu akakupenda zaidi,” alisema.

Bw Muramba alisema ilikuwa uamuzi mgumu kuamua ni nani atapeperusha bendera ya chama uchaguzini baina ya wagombeaji hao watatu.

Haya yalijiri huku Bi Jumwa akimpigia Bw Omar debe harusini eneo la Ganda.

You can share this post!

Wakuu wa jela wahamishwa kashfa ikizuka

Simanzi maziko ya wahanga 68 wa ajali ya mafuta yakianza TZ

adminleo