Michezo

Rwanda yajiandaa kuchuana na Kenya U-20 Kombe la Afrika

March 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Rwanda imeanza mazoezi Jumatano tayari kupepetana na Kenya katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika la Under-20 mwaka 2019, gazeti la New Times limeripoti. Junior Wasps jinsi inafahamika kwa jina la utani, inafanyia mazoezi yake uwanjani Amahoro.

Mechi ya mkondo wa kwanza kati ya Kenya na Rwanda ni kati ya Machi 30 na Aprili 1 nchini Kenya, huku ile ya marudiano ikipangiwa kuchezwa jijini Kigali kati ya Aprili 20 na Aprili 22.

Gazeti hilo, ambalo Machi 17 lilichapisha habari kwamba ziara ya Rwanda nchini Kenya inaning’inia kutokana na ukosefu wa fedha, limenukuu kocha Vincent Mashami akisema, “Tunaanza kujiandaa Jumatano.”

Mashami amejumuisha mabeki wa APR Prince Buregeya na Shaffy Ngaboyisonga na mvamizi Lague Byiringiro katika kikosi chake pamoja na kiungo wa Rayon Sports, Alitijan Tumushime, gazeti hilo limesema.

Mshindi kati ya Kenya na Rwanda atajikatia tiketi ya kupambana na mabingwa wa Afrika Zambia katika raundi ya pili mwezi Mei.

Raundi ya tatu, ambayo itaandaliwa Julai, itaamua timu zitakazoshiriki Kombe la Afrika mwaka 2019 nchini Niger. Rising Stars ya Kenya imekita kambi jijini Nairobi ikijiweka tayari kwa pambano hili.

Kikosi cha Rwanda:

Makipa – Cyuzuzo (Unity), Fiacre Ntwali (Intare) na Eduard Iratugenera (Mukura);

Mabeki – Shaffy Songayingabo (APR), Prince Buregeya (APR), Christian Ishimwe (Marines), Placide Aime Uwineza (SC Kiyovu), Marc Nkubana (Unity), Govin Nshimiyimana (Intare), Oliver Habineza (Rayon Sports), Tresor Ndabarasa (Unity), Felicien Hakizimana (Intare) na Clement Niyigena (Intare);

Viungo – Saleh Nyirinkindi (APR), Janvier Bonane (SC Kiyovu), Bogarde Cyitegetse (Bugesera), Alitijan Tumuhime (Rayon Sports), Fred Muhozi (AS Kigali), Saleh Ishimwe (Unity), Jacob Byukusenge (Intare), Charles Nyandwi (Intare), Emmanuel Uwimana (Intare) na Jean Paul Nduwayezu (Musanze);

Washambuliaji – Lague Byiringiro (APR), Patrick Mugisha (Marines), Protais Sindambiwe (Intare), Gilbert Nshimyumuremi (Intare), Aloysias Tumusime (Intare) na Emmanuel Fleury Ndayisenga (Mukura).