Operesheni ya Matiang’i yang’oa nanga Pwani
MOHAMED AHMED na KALUME KAZUNGU
AGIZO la Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuhusu vita dhidi ya mihadarati limeanza kutekelezwa na polisi Pwani.
Dkt Matiang’i aliahidi Jumapili kwamba msako mkali utaanzishwa kunasa walanguzi wa dawa za kulevya kwani wamehusishwa na uhalifu ambao umekithiri hasa Kaunti ya Mombasa.
Jumatatu, makachero zaidi ya 20 walivamia nyumba ya kifahari ya bwanyenye Ali Punjani mtaani Nyali mwendo wa saa nane mchana.
Diwani wa Wadi ya Bofu iliyo eneobunge la Likoni, Bw Ahmed Salama almaarufu kama Bulldozer naye alikamatwa kwa kuhusishwa na ulanguzi wa mihadarati Mombasa.
Naye OCS wa Kizingitini katika Kaunti ya Lamu, Shadrack Mumo alikamatwa kwa kuachilia mshukiwa wa ulanguzi pamoja na shehena yake ya bangi.
Polisi walioenda kumkamata Punjani walishindwa kuingia ndani ya nyumba hiyo baada ya kukita kambi kwa zaidi ya saa mbili kwani hawakufunguliwa mlango.
Operesheni hiyo iliongozwa na Kamanda wa Kaunti, Bw Johnson Ipara na Mkuu wa DCI Mombasa, Bw Anthony Muriithi.
Ripoti ya polisi ambayo Taifa Leo iliona, ilisema gari jeupe la mmoja wa jamaa za Punjani anayefahamika kama ‘Macho Nne’ iliondoka hapo nyumbani ikielekea Kwale, huku ikidaiwa Punjani alisafiri India.
Duru zilisema msako huenda ukanasa wafanyabiashara mashuhuri, wanasiasa na viongozi wengine wenye ushawishi katika jamii.
Bw Punjani hudaiwa kuhusiana kibiashara na familia ya Akasha, ambayo jamaa zao wanasubiri kuhukumiwa Amerika baada ya kupatikana na hatia ya ulanguzi wa mihadarati.
Kwenye kesi ya Baktash na Ibrahim Akasha iliyosikilizwa Amerika, shahidi mkuu Vijay Goswami alidai Bw Punjani alikuwa mshindani wao katika biashara hiyo haramu.
Huku hayo yakijiri, Afisa Msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Kizingitini (OCS), Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki, Bw Shadrack Mumo alikamatwa kwa kuchukua hongo ya Sh50,000 ili kuachilia shehena ya dawa za kulevya iliyokuwa imenaswa eneo la Mtangawanda mnamo Jumapili.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Bw Muchangi Kioi alisema OCS huyo pia alimwachilia huru mshukiwa mkuu wa ulanguzi kwa jina Swabri, ambaye alikuwa amekamatwa akiwa na shehena hiyo ya bangi.