• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
Waislamu watishia kususia sensa wakidai kuna ubaguzi

Waislamu watishia kususia sensa wakidai kuna ubaguzi

Na GAITANO PESSA

WAISLAMU katika eneobunge la Budalang’i, Kaunti ya Busia wametishia kususia zoezi la sensa linalotarajiwa kuanza juma lijalo.

Wakiongozwa na Imam wa msikiti wa Marenga, Sheikh Abdul Aziz Mohammed, waumini wa dini hiyo walidai baadhi ya majina yao yaliondolewa katika orodha ya wale waliotarajiwa kusimamia zoezi hilo licha ya kufuzu.

Akiwahutubia waumini waliofika katika msikiti huo kwa maadhimisho ya Idd-ul-Adha mnamo Jumapili, Sheikh Aziz alidai kuwa hakuna jina hata moja la Muislamu lililoorodheshwa katika orodha ya wale watakaosimamia zoezi hilo kutoka eneobunge hilo.

“Inavunja moyo kuwa serikali imetutenga kama jamii katika zoezi hili. Iweje kuwa hamna hata jina moja la MuIslamu lililoorodheshwa miongoni mwa wale watakaosimamia sensa ya mwaka huu. Tunataka serikali ituhusishe katika mipango yake la sivyo hatutajitokeza kuhesabiwa iwapo waumini wa dini yetu hawataorodheshwa katika zoezi hilo kabla ya kungo’a nanga Agosti 24,” alisema.

Aidha alihoji kuwa ingawa zoezi hili ni muhimu kwa taifa, uajiri wa wasimamizi ulifanywa kinyume cha matarajio yao.

Kuhusu jinamizi la ufisadi, sheikh Aziz alitoa wito kwa wabunge kupitisha sheria zinazozipa mahakama kutoa hukumu kali dhidi ya washatakiwa ikiwemo kukatwa kiungo chake cha mkono.

Serikali tayari imetangaza hatua kabambe za kusimamia shughuli hiyo, ambazo ni pamoja na kuhakikishia Wakenya usalama wa kutosha.

Wizara ya Elimu pia imebadilisha tarehe za shule kufunguliwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanahesabiwa wakiwa makwao.

Vile vile, kuna pendekezo la siku hiyo kutangazwa kama likizo ili kuhakikisha kuwa Wakenya wote wanapata fursa ya kuhesabiwa wakiwa nyumbani.

You can share this post!

Viongozi Rift waikemea serikali kujaribu kufurusha familia...

Mbunge maalum ataka Munya ajiuzulu

adminleo