WASONGA: Matiang'i ajue mbinu za kisasa za walanguzi
NA CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i mnamo Jumapili alitangaza kuwa serikali imeanzisha upya vita dhidi ya dawa za kulevya katika Pwani ya Kenya, akitaja mihadarati kama sababu kuu ya vijana kujiunga na magenge ya uhalifu.
Lakini uuzaji wa mihadarati kote nchini umekuwa mwiba kwa serikali, na hivyo haifai kupiga kambi eneo moja tu kwa sababu kumekuwa na ripoti za mihadarati katika meaneo mengine nchini ambako mbinu tofauti hutumika kufanikisha biashara hiyo haramu.
Na gazeti la Taifa Leo mwezi uliopita lilichapisha makala kuhusu mbinu mpya zinazotumiwa na walanguzi wa dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Mbinu hizo zinajumuisha kutumia wanawake wazee kusafirisha mihadarati, watoto, mavazi ya kidini, magari ya wanasiasa na serikali, yale ya kusafirisha bidhaa maalumu na wakati mwingine kutumia walemavu.
Kulingana na ripoti ya Afisi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia masuala ya Mihadarati na Uhalifu, wakati mwingi walanguzi hutumia wanawake ambao wako katika hali mbaya kimaisha na huhitaji usaidizi wa kifedha kwa dharura.
Lakini wakati mwingine, wao wenyewe ndio walanguzi halisi baada ya kujifunza biashara hiyo kwa muda.
Katika Kaunti ya Murang’a ambapo idadi ya vijana wanaoathiriwa na utumizi wa dawa za kulevya na pombe haramu imeongezeka kwa kasi, kuna watu wanaovaa vilemba vya Akorino na kofia za Rasta kuficha bangi vichwani mwao.
Aprili mwaka uliopita, maafisa watatu wa Shirika la Ukusanyaji Ushuru (KRA) walikamatwa wakiwa na kiwango kikubwa cha dawa za kulevya aina ya Mandrax katika Uwanja wa Ndege wa Eldoret.
Walikuwa wameficha dawa hizo katika mifuko ya kufungia vitamini za kuongeza nguvu mwilini. Walichukuliwa hatua gani?
Hii ndiyo hali halisi katika biashara haramu ya bangi, Cocaine, Heroin na Mandrax humu nchini. Hivyo, ili kuwakabili walanguzi, serikali yafaa kuanzisha operesheni kote nchini.
Dkt Matiang’i anafaa kutumia zaidi ya mbinu wanazotumia walanguzi kuhepa mkono wa sheria, iwapo analenga kuzima uovu huu.
Ni wazo zuri kuwalinda wanachi dhidi ya magenge yanayowahangaisha, lakini ili kushinda vita dhidi ya dawa za kulevya, serikali itahitaji kuwatuma maafisa wa polisi katika kaunti mbalimbali, na kuwapa mafunzo kuhusu mbinu ibuka za kuuza mihadarati zinazotumika.
Wakati mwingine, uovu huu unaendelezwa na maafisa serikalini. Je, Dkt Matiang’i anajua hili? Anajua magari ya serikali yanatumika kusafirisha mihadarati? Anajua walemavu wanatumiwa katika mchakato huo? Ni nini kinawasukuma vijana kujihusisha na mihadarati?
Ikiwa serikali inajua majibu ya maswali haya kwa kina, basi vita vyake dhidi ya mihadarati vitafanikiwa. Iwapo haitambui mbinu mpya wanazotumia walanguzi, basi juhudi zake zitakuwa tu kama za awali ambapo ziligonga mwamba.