• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
Viongozi Rift waikemea serikali kujaribu kufurusha familia 60,000 Mau

Viongozi Rift waikemea serikali kujaribu kufurusha familia 60,000 Mau

NA GEOFFREY ONDIEKI

Baadhi ya viongozi wa Bonde la ufa wamelaani vikali tishio la serikali kutaka kuzifurusha zaidi ya familia 60,000 ambazo zinaishi katika msitu wa Mau.

Wakiongozwa na Seneta wa Baringo Gideon Moi, viongozi hawa wameitaja hatua hiyo kuwa ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.

“Hatua ya kuzifurusha familia hizo itaathiri zaidi ya wanafunzi 8,000 na kati yao 1,000 ni watahiniwa wa mtihani wa kitaifa,” alisema seneta Moi.

Aidha Seneta Moi badala yake aliitaka serikali kufanya mazungumzo na familia hizo ili kumaliza mgogoro unaoshuhudiwa.

“Serikali inafaa kufanya mkutano kati ya jamii za Maa na Kalenjin na kutafuta suluhu ya kudumu,” alisema Bw Moi.

Aliongeza kuwa kuziondoa familia hizo kutoka Mau itasababisha athari kubwa kwa familia husika.

Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos aliitaka serikali kutafuta njia mbadala kusuluhisha mgogoro huo, ikiwemo kuwapa fidia wakazi hao badala ya kuwaondoa kwa nguvu.

“Serikali inafaa kufikiria kuwapa fidia wakazi hao kwa kununua mashamba hayo yote na kuwatafutia mahalI mbadala pa kuishi. Hiyo itakuwa na afueni kuliko kuwafurusha bila fidia,” alisema Gavana Tolgos.

Gavana Tolgos alisema kuwa kaunti yake bado inashuhudia changamoto sawia na hizo pale ambapo mamia ya familia waliondolewa kutoka msitu wa Embobut bila fidia. Alisema familia hizo kwa sasa zinaishi hali duni ikizingatiwa wanapata wakati mgumu kujikimu.

Upande wake aliyekuwa mbunge wa Kipkelion Magerer Lagat, alionya kuwa mpango wa kuzifurusha familia ni kuhatarisha maisha ya maelfu na ni kinyume na haki za kibinadamu.

“Watoto wasio na hatia watateseka sana iwapo mpango huo hautasitishwa,” alisema Bw Lagat.

Bw Lagat aliongeza kuwa haimaanishi kuwa wapo kinyume na utunzaji wa mazingira, ila wanaomba kuwe na utaratibu mwafaka wa kuziondoa familia hizo. Alihimiza serikali kukumbatia mazungumzo kutatua mgogoro huo.

“Elimu ya wanafunzi itaathiriwa sana na hivyo itaharibu maisha ya baadaye ya watoto wetu,” alisema.

Aliyekuwa Mbunge wa Eldama Ravine Musa Sirma alikiri kuwa maisha ya binadamu yanafaa kupewa kibao mbele kabla kuchukua uamuzi wa kuwafurusha wakazi wa msitu wa Mau. “Wakazi wa Mau sio wanyama pori.Wanafaa kutolewa kwa utaratibu unaofaa na sio kuwafurusha kwa nguvu,” alisema Bw Sirma.

Bw Sirma alisema kuwa suala la msitu wa Mau halistahili kutiwa siasa ikizingatiwa viongozi wengi hutumia kujiimarisha kisiasa.

Katibu mkuu wa chama cha KANU Nick Salat alikiri kuwa msitu wa Mau kila mara unatumiwa na wanasiasa kupiga domo bila suluhisho. Aliitaka serikali kutafuta suluhu ya kudumu mara moja.

“Tutatembea na watu wa Mau hadi mwisho,na tunataka wanafunzi wao wafanye mtihani hapo,” alisema Bw Salat.

Aliongeza kuwa jamii ya Kalenjin iko tayari kwa mazungumzo ili kutafuta suluhu.-

Matamshi haya yanajiri siku chache baada ya Waziri wa mazingira Kiriako Tobiko alitangaza serikali itaanza mchakato wa kuziondoa familia zinazoishi katika msitu wa Mau.

Bw Tobiko alionya kuwa serikali haitawafidia wakazi hao akisema kuwa waliingilia msitu huo kwa njia haramu.

You can share this post!

Wanafunzi waliotia fora tamashani kumtumbuiza Ruto

Waislamu watishia kususia sensa wakidai kuna ubaguzi

adminleo