• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Polisi waendesha msako wa walanguzi wa dawa Pwani

Polisi waendesha msako wa walanguzi wa dawa Pwani

Na WAANDISHI WETU

MKEWE bwanyenye wa Mombasa, Ali Punjani alitiwa mbaroni na polisi Jumanne wakati wa operesheni kwenye nyumba yao eneo la Nyali, Mombasa.

Maafisa hao walimkamata Bi Karki Sushmi Ja, 24, wakati wa msako huo unaohusiana na madai kwamba Bw Punjani anahusika katika biashara haramu ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Bi Ja alikamatwa pamoja na raia wengine wawili wa kigeni wakiwa wamejificha katika jumba hilo la kifahari.

Kamanda wa polisi kaunti ya Mombasa, Bw Johnston Ipara ambaye alikuwa akiongoza operesheni hiyo alisema kuwa washukiwa hao watahojiwa kuhusiana na biashara za Bw Punjani.

Msako huo uliendeshwa huku mahakama ikikataa kumzuilia Mwakilishi wa Wadi kwa siku tatu.

Hakimu Mwandamizi wa Mombasa, Edgar Kagoni, alisema ombi kuwa Bw Ahmed Salama Omar azuiliwe ili polisi wakamilishe uchunguzi halikuwa na msingi wowote kisheria.

Hata hivyo, hakimu alimuaru Bw Omar ashirikiane na polisi.

“Mchunguzi wa kesi Bw Charles Onyango amesema hakuna dawa zozote za kulevya zilizopatikana wala hakuna shahidi aliyenakili taarifa. Kwa hivyo hakuna uwezekano wa kuhitilafiana na mashahidi,” alisema Bw Kagoni.

Katika ombi lao, polisi walitaka kupewa siku tatu kumzuia Bw Omar ambaye alikamatwa Jumatatu, ili wamalize uchunguzi.

Kupitia wakili Yusuf Aboubakar, mwakilishi huyo wa wadi ya Bofu alipinga ombi hilo akisema kuwa ilikuwa ni njama ya kisiasa dhidi yake.

Kesi ya Bw Omar ni miongoni mwa nyingine zaidi ya kesi 30 zilizofikishwa kortini, siku mbili baada ya waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i kutangaza vita dhidi ya dawa a kulevya, alizotaja kuwa chanzo cha kukithiri kwa magege ya ujambazi.

Kesi 15 zilisomwa katika mahakama ya Shanzu huku mahakama ya Mombasa ikinakili kesi 17 za washukiwa wa dawa mbalimbali za kulevya huku nusu yao ikiwa heroini na nusu iliyobaki ikiwa ni wale wa bangi na kokeni.

Jaffar Mwinyihajji alipatikana na gramu 200 za heroini katika maeneo ya Mtwapa Kaunti ya Kilifi mnamo Agosti 12. Gramu hizo zilikadiriwa kuwa na thamani ya Sh100,000.

Katika kaunti ya Lamu, Kamanda wa Polisi, Bw Muchangi Kioi, aliwataka washukiwa wajisalimishe mara moja au majina na sura zao zichapishwe na kutangazwa kwa umma.

Bw Kioi aliwataka wakazi wenye taarifa kuwahusu baadhi ya maafisa wa polisi ambao wamekuwa wakishirikiana na walanguzi wa dawa za kulevya kuripoti maafisa hao ili wakamatwe na kukabiliwa na mkono wa sheria.

Jumatatu, Afisa Msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Kizingitini, Shadrack Mumo alikamatwa na polisi baada ya kuchukua hongo ya Sh 50,000 ili kuachilia shehena ya dawa za kulevya aina ya bangi iliyokuwa imekamatwa eneo la Kizingitini, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki Jumapili.

Afisa huyo atafikishwa mahakamani juma hili.

Ripoti za AHMED MOHAMED, PHILIP MUYANGA, MISHI GONGO na KALUME MAZUNGU

You can share this post!

Wito maoni ya BBI na ‘Punguza Mizigo’ yaunganishwe

Kioja maafisa wa kaunti kufukua maiti na kuivua sare za kazi

adminleo