Saba wasakwa eneo la Makwa kwa kutajwa utengenezaji pombe haramu
Na LAWRENCE ONGARO
WATENGENEZAJI saba wa pombe haramu eneo la Makwa, Gatundu Kusini wanasakwa na polisi ili wafikishwe mahakamani na kufunguliwa mashtaka.
Kamishna wa Kaunti ya Kiambu, Bw Wilson Wayanga alitoa amri hiyo Jumanne akisema watengenezaji hao ni hatari kwa maisha ya binadamu.
Wakazi wa kijiji cha Makwa wanazidi kulalamika kuwa pombe haramu imerejea kwa kishindo huku vijana wengi wakiwa tayari wameathirika vibaya.
Bw Wanyanga alikuwa ameandamana na wakuu wa serikali na machifu wote wa eneo hilo.
“Watengenezaji pombe wameharibu kabisa maisha ya vijana katika eneo hili,” alisema Bw Wanyanga.
Alisema uchunguzi uliofanywa umedhibitisha kuwa maeneo yaliyoathirika kabisa na pombe haramu ni Mwea, Gatukuyu, Mang’u, na vitingoji vyake.
Wakazi hao waliohudhuria baraza lililoandaliwa na Kamishna huyo, walionekana kujawa na ghadhabu huku wakitaka hatua ya haraka ichukuliwe ili kudhibiti unywaji wa pombe haramu.
Mkazi mmoja wa eneo hilo, Bw Peter Chege, alipendekeza maafisa wa usalama ambao wametumikia serikali eneo hilo kwa muda mrefu wapewe uhamisho bila kuchelewa.
“Tunaelewa kuna maafisa wengi wa serikali ambao hushirikiana na watengenezaji pombe; jambo ambalo limeponza kabisa juhudi za serikali kukabiliana na pombe haramu,” alisema Bw Chege.
Kufika kujionea
Bw Wanyanga alisema watafanya juhudi kuzuru eneo hilo angalau mara moja kila wiki ili kujionea kazi ambayo inaendeshwa na maafisa wa serikali.
“Nitafika hapa kila wiki ili kujionea jinsi machifu na maafisa wa serikali wanavyopambana ili kuangamiza pombe haramu,” alisema afisa huyo.
Alisema kila naibu chifu na machifu wenyewe watalazimika kuzunguka vijijini ili kupambana na pombe haramu na dawa za kulevya.
“Kila mmoja atalazimika kuchunga eneo lake na kuwasilisha ripoti katika ofisi yangu kila wiki,” alisema Bw Wanyanga.
Mzee mmoja wa kijiji hicho Bw Michael Muchai alisema licha ya ukweli kwamba pombe hiyo ilikuwa imekabiliwa vilivyo, bado kuna watengenezaji wachache ambao “ni sugu.”
“Sisi tunaiomba serikali kufanya hima ili kuokoa vijana wetu ambao wametekwa nyara na pombe hiyo haramu. Tutahakikisha tunaungana kama wakazi ili kupambana nao,” alisema Muchai.
Naye mwanamke mmoja mkazi wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake lichapishwe, alisema vijana wao wengi wameathirika na wangetaka serikali kuingilia kati.
“Hatutakubali waje hapa kutuharibia vijana hapa Makwa. Sisi wakazi wa hapa tutaungana kuona ya kwamba pombe hiyo imeangamizwa kabisa,” alisema mama huyo.
Alionyesha mkono wake uliokatwa na mmoja wa wapikaji pombe haramu kwa sababu ya kile alikitaja ni “kukosoa mienendo yao.”