Watatu wamezea mate kiti cha Kibra
LEONARD ONYANGO na JUSTUS OCHIENG
SPIKA wa Bunge Justin Muturi ametangaza kiti cha ubunge cha Kibra kuwa wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth mwezi uliopita.
Bw Muturi, kupitia notisi katika Gazeti Rasmi la Serikali, aliitaka Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) kuanza harakati ya kuandaa uchaguzi mdogo katika eneobunge la Kibra.
Kulingana na sheria, tume ya IEBC sasa ina muda wa siku 90 kuandaa uchaguzi mdogo Kibra.
Wakati huo huo, mwandani wa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, Bw Eliud Owalo amejiuzulu kutoka kwa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na kujiunga na kile cha Amani National Congress chake Musalia Mudavadi.
Hatua hiyo imeonekana kuwa maandalizi ya kuwania kiti hicho cha Kibra.
Bw Owalo aliongoza kamati ya kampeni za urais za Bw Odinga 2013 .
Katika uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Owalo alishindwa na Okoth kwenye mchujo wa ODM.
Ndugu mdogo wa Okoth, Imran, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna ni mwa watu wanaomezea mate kiti hicho.
Mbunge wa zamani wa Kasarani, Elizabeth Ongoro pia anadaiwa kuwa mbioni kumrithi Okoth.
Kinara wa ODM Raila Odinga atakuwa na kibarua ikiwa atampatia tiketi ya chama hicho fursa ya kumrithi nduguye au ataelekeza tiketi kwa Bw Sifuna.
Kadhalika, haijulikani ikiwa chama cha ODM kitafanya kura za mchujo au mwaniaji atapewa tiketi moja kwa moja.