• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 PM
Raila njia panda washirika wake wakimezea ubunge Kibra

Raila njia panda washirika wake wakimezea ubunge Kibra

Na CECIL ODONGO

KINARA wa Chama cha ODM Raila Odinga anakabiliwa na mtihani mgumu wa kisiasa kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa katika eneobunge la Kibra huku wandani wake wa kisiasa wakizidi kutajwa kama wanaomezea mate kiti hicho kilichosalia wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth.

Kampeni tayari zimeshika kasi katika eneobunge hilo, baadhi ya wawaniaji wakijipendekeza kwa wapigakura baada ya Spika wa Bunge Justin Muturi kutangaza kiti hicho kuwa wazi Jumanne.

Tangazo la Bw Muturi sasa linaipa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ruhusa ya kuandaa uchaguzi kwenye eneobunge hilo ndani ya siku 90.

Bw Odinga ambaye alikuwa mbunge wa eneo hilo kuanzia mwaka wa 1992 hadi 2013 atalazimika kujikuna kichwa zaidi katika kuamua iwapo chama cha ODM kitaandaa uchaguzi wa mchujo au kumteua mgombeaji moja kwa moja jinsi ilivyofanya kwenye chaguzi ndogo za Embakasi Kusini na Ugenya.

Miongoni mwa wanaotajwa kuwa wanamezea mate kiti hicho cha Kibra ni Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna, aliyekuwa mbunge wa Embakasi Kusini Irshad Sumra, Kiongozi wa vijana wa ODM eneo la Kibra Benson Musungu, Mjane wa Ken Okoth, Bi Monica, wanawe Bw Odinga, Bi Rosemary na Winnie, Imran Okoth aliye nduguye marehemu na mbunge wa zamani wa Kasarani Elizabeth Ongoro.

Mshauri wa zamani wa masuala ya kisiasa wa Bw Odinga, Bw Eliud Owalo pia ametajwa miongoni mwa wanaomeza mate wadhifa huo. Bw Owalo alijiuzulu kutoka ODM wiki hii na kujiunga na ANC inayoongozwa na Musalia Mudavadi katika kile ambacho wadadisi wa kisiasa wanasema ni kujiweka pazuri kuwania kiti hicho.

Duru pia zinaarifu kwamba baadhi ya wabunge na maafisa wa chama wametofautiana kuhusu nani wa kuungwa mkono na chama kati ya Bi Ongoro na Bw Okoth.

Kulingana na mdadisi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, Bw Odinga atalazimika kubadilisha mbinu zilizosababishwa kushindwa kwa wawaniaji wa ODM kwenye chaguzi za Ugenya na Embakasi Kusini kwa kuhakikisha kuwa demokrasia inazingatiwa wakati wa mchujo kisha kuibuka na mgombeaji bora anayeshabikiwa na wote.

“Kura ya mchujo yenye uwazi ndiyo njia bora ya kuibuka na mwaniaji bora wa chama cha ODM eneo la Kibra. Kwa kuwa hii ni ngome yake ya kisiasa, Bw Odinga anafaa kumakinika na kuwapa raia fursa ya kumchagua mwaniaji wa ODM. Kibarua kigumu hata zaidi ni kuwapuuza wandani wake na kuwazuia kuingilia kura ya mchujo,” anasema Bw Andati.

Kulingana naye, wananchi watazingatia rekodi ya maendeleo ya mwaniaji huku pia masuala ya kitamaduni yaliyozingira mazishi ya Bw Okoth na miegemeo ya kisiasa ya jamii mbalimbali zinazoishi eneobunge hilo yakichangia ushindi wa mmoja wa wawaniaji hawa.

You can share this post!

Ushoga waeneza Ukimwi magerezani

Serikali ya Oparanya kujadili ripoti ya kufufua Mumias...

adminleo