• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Viongozi wahimiza raia wajitokeze kwa sensa

Viongozi wahimiza raia wajitokeze kwa sensa

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI mbalimbali wamewahimiza wananchi wajitokeze kwa shughuli ya kuhesabiwa katika muda wa wiki mbili zijazo.

Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui alisema, shughuli hiyo ni muhimu kwa sababu itasaidia kujua idadi kamili ya watu na pia kutambua sehemu ambazo zinahitaji kuboreshwa kwa haraka.

“Watu wote, wakubwa kwa wadogo, watahesabiwa usiku wa Agosti 24 na yule ambaye hatafikiwa wakati wa shughuli hiyo basi na aripoti mara moja,” akasema Bw Kinyanjui.

Aliongeza kuwa, kina mama watakao jifungua siku hiyo wahakikishe pia watoto wao wamehesabiwa.

“Hesabu kamili ya watu wa eneo fulani ndio huwezesha sehemu hiyo kupata fedha nyingi za maendeleo kutoka kwa serikali kuu,” akasema Bw Kinyanjui huku akiongeza kila mkazi ahakikishe anajibu maswali yote yatayoulizwa na kwa njia ya ukamilifu bila kukosea.

Kamishina wa Nakuru Bw Erastus Mbui alisema usalama utaimarishwa siku hiyo kuanzia mjini hadi mashinani.

“Tuna ufahamu kuwa majambazi huenda wakatumia nafasi hiyo kuingia kwenye nyumba za watu na kuwaibia. Hatutaruhusu hayo kutendeka,” akasema Bw Mbui na kuwaonya wakazi kuwa macho na kuripoti kwa polisi visa vyovyote vya kutatanisha.

Mwenzake wa Pokot Magharibi, Prof John Lonyangapuo, ameitaka serikali ihakikishe wakazi kutoka kaunti zinazopakana na nchi jirani ya Uganda waliohama kutafuta maji na nyasi wanahesabiwa.

Mnamo Jumatano, gavana huyo alizuru kijiji cha Natekol nchini Uganda kuwarai wafugaji wa jamii ya Pokot warejee nyumbani na kuwahamasisha kuhusu umuhimu kuhesabiwa.

“Tutafanya mipango kubadilisha wachungaji siku hiyo ya kuhesabiwa. Usichelewe kuhesabiwa. Rudini nyumbani ili mhesabiwe,” akasema.

Mjini Mombasa, watu wenye jinsia mbili (Huntha) wametakiwa wajitokeze bila kuona aibu kwa shughuli ya kuhesabiwa.

Kamishna wa tume ya marekebisho ya sheria ya Kenya, Bw Mbage Njuguna, alisema kufikia sasa watu wa jinsia mbili wanapitia changamoto nyingi ikiwemo kukosa stakabadhi muhimu kama vile hati ya kuzaliwa, vitambulisho na zile za kusafiri.

“Wanapitia aibu kufuatia mtoto kuandikishwa kwa jina la kike kisha jinsia kubadilika anpopevuka, jambo hili linawafanya mara nyingi kujipata upande mbaya wa sheria na hata kulazimika kujieleza jambo ambalo ni aibu,”alieleza.

Bw Njuguna alisema sheria itawaruhusu kubadilisha majina katika hati muhimu kama kitambulisho na zile za kusafiria, pindi wanapopevuka na kujipata tofauti na jinsia waliyokuzwa nayo.

“Wanapozaliwa ni vigumu kwa madaktari kuthibitisha jinsia zao, jambo linalopelekea wazazi kuwapa majina kulingana na jinsia wanayotaka bila kujua ni jinsia gani iliyozidi nyingine,”alisema.

Alisema jambo hili hupelekea wao kutengwa na hata kukejeliwa na watoto wenzao,”aliongeza.

Ripoti za PHYLLIS MUSASIA, OSCAR KAKAI na MISHI GONGO

You can share this post!

Sh100m: Ouko kuchunguza ziara ya wabunge Amerika

Wahimizwa wasibague mahabusu wa zamani

adminleo