Mwanga wa matumaini Sudan
Na AFP
KHARTOUM, Sudan
MWANGA wa matumaini umeangaza nchini Sudan huku viongozi wa kijeshi na viongozi wa makundi ya waandamanaji wakitazamiwa kutia saini mkataba muhimu kesho Jumamosi.
Mkataba huo ulioafikiwa kufuatia ghasia za kikatili za uasi, unalenga kuanzisha utawala wa kiraia.
Hafla hiyo pia itajumuisha kutangazwa rasmi kwa nakala ya Katiba iliyoandikwa mnamo Agosti 4, 2019, kati ya baraza la kijeshi linalotawala nchini humo na muungano wa upinzani, Alliance for Freedom and Change.
Mkataba huo ulikomesha ghasia za karibu miezi minane ambapo umma uliandamana dhidi ya Rais Omar al-Bashir aliyeng’atuliwa mamlakani mnamo Aprili baada ya kutawala kwa miaka 30.
Maafikiano yaliyowezeshwa na Muungano wa Afrika na Ethiopia, yalipokelea kwa furaha na pande zote huku waandamanaji wakisherehekea walichoona kama ushindi wa “mageuzi” yao nao majenerali wakijipiga kifua kwa kuzuia mapigano ya kikabila.
Japo maafikano hayo yanatimiza sehemu kubwa ya matakwa ya kambi ya waandamanaji, masharti yake yanaliacha jeshi na mamlaka makubwa huku serikali mpya ya raia ikiachiwa changamoto tele.
Huku kukiwa na masuala mengi ambayo bado hayajashughulikiwa, waangalizi walionya kwamba bado ni mapema sana kutaja matukio ya hivi majuzi kama “kufaulu kubadilisha utawala.”
“Mwelekeo wa siasa utakuwa na maana zaidi kushinda vijikaratasi,” alisema Rosalind Marsden kutoka shirika la Think Tank la Chatham House Uingereza.
Akaongeza: “Changamoto kuu litakalokabili serikali litakuwa kubomoa taifa lililokita mizizi la kiislamu lililodhibiti taasisi zote za kitaifa na sekta muhimu za uchumi, ikiwemo mamia ya biashara zinazomilikiwa na vikosi vya kijeshi.”
Kufuatia hatua hiyo ya kutia sahihi rasmi nakala za kubadilisha mamlaka, Sudan itaanza mchakato utakaojumuisha hatua muhimu za kwanza.
Baraza jipya la mpito la utawala wa kiraia litatangazwa Jumapili, ikifuatiwa na kumtaja waziri mkuu siku mbili baadaye.
Mnamo Alhamisi, viongozi wa waandamanaji walikubaliana kumteua aliyekuwa afisa wa Umoja wa Mataifa, UN, Abdalla Hamdok, kama waziri mkuu.
Mtaalamu huyo wa uchumi kwa muda mrefu aliyejiuzulu mwaka jana kama naibu katibu mkuu wa Tume ya UN kuhusu Uchumi Afrika, anatazamiwa kuchaguliwa rasmi mnamo Agosti 20, kwa mujibu wa taarifa hiyo.
Baraza la utawala litakaloundwa katika muda wa miezi mitatu litajumuisha angalau asilimia 40 wanawake, kuashiria nafasi muhimu waliochangia wanawake katika kambi ya maandamano.
Imetafsiriwa na Mary Wangari