• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
KINAYA: Kumbe Waamerika walitaka ‘mtu’ wa kuwapigia wengine makalioni!

KINAYA: Kumbe Waamerika walitaka ‘mtu’ wa kuwapigia wengine makalioni!

Na DOUGLAS MUTUA

WATU wana utani kweli!

Rafiki yangu wa miaka mingi kwa jina Mutinda Munyao, ambaye ni mhariri wa magazeti yetu ya Kiingereza, nusura anitegue mbavu.

Anatania kuhusu kila kitu, kila mtu na kila hali. Naam! Hata yanayokuliza yanamchekesha wakati mwingine. Hatimaye atakuauni lakini.

Juzi nimekutana naye akanicheka kwa kuishi nchi ya mja ambaye, japo hajachunguzwa, kila dalili inaonyesha kuna kitu kisicho sawa akilini.

Rafiki yangu huyo ameniambia Donald Trump ni kama mwendawazimu anayeingia nyumbani kwako na kuanza kufagia hapo nje.

Unajua si vizuri kwa mwehu kujituma kufagia kwako, lakini hutaki kumkataza. Nje pachafu, unataka taka ziondolewe.

Anafanya kazi nzuri ambayo mwenyewe umetaka kuifanya ila ukazembea, lakini hafai. Ni kichaa. Unamwogopa. Hujui umfanyie nini.

Una afua mbili: Ama umshangilie na kumlimbikizia sifa kwa kazi njema au unyamaze kabisa, ujionee anavyofanya kazi. Uko kwenye njia panda.

Ndipo Waamerika walipo. Na wamegawanyika mno! Wapo wanaomshangilia Rais wao kwa kufanya kazi ‘njema’ ya kumchukia na kumbugudhi kila asiyefanana nao.

Wapo pia wanaomtazama kimyakimya, wanatambua kimoyomoyo kazi ‘nzuri’ anayofanya, lakini hawawezi kumkataza. Wamkatazeje ilhali anawafaa?

Walitamani kwa mioyo yao yote wampate fahali wa kazi kama huyu, mja mfidhuli asiyeogopa yeyote wala chochote, aliyejaaliwa jeuri akanyimwa fedheha ya kuitekeleza.

Wapo wahafidhina wa kweli ambao ni wabaguzi wa rangi kindakindaki, hata uwatilie dua, ufuatishe na mfungo, unafanya kazi bure. Hawabadiliki. Hawaogopi. Na hawajifichi.

Ukiwahesabu hao ili kukadiria umaarufu wa Trump, uwalinganishe na wale wanaokaa kimya tu au kujifanya hawampendi, utadanganyika.

Hao ndio watu wanaohojiwa na kampuni za tafiti za maoni na kuupotosha ulimwengu kwa kuuambia huyo bwana hawezi kumshinda yeyote kwenye uchaguzi.

Ole wako ukiwaamini! Utaamshwa na mwangwi wa mwanguko wa anayeshindana na Trump kura zikihesabiwa!

Kisa na maana? Waliodai kutompenda walifanya mambo yao walipoingia kwenye chumba kidogo cha kupigia kura wasikoonena na mtu.

Wamarekani ni watu wa kuchekesha. Na sizungumzii Wazungu pekee, la hasha! Nawarejelea hata waliochukua uraia hiyo jana.

Wote kwa muda mrefu sana wametamani kumpata kiongozi atakayewazuia watu zaidi kuwa Wamarekani au hata kuhamia huko tu kufanya kazi.

Yaani mtu akiingia anataka milango ifungwe, watu weupe, weusi, wekundu, wa manjano na kadhalika waliomo watoshe, ikibidi baadhi yao waondolewe, ila wasiingie wengine.

Ni fikra za kipumbavu na kibinafsi zinazomhadaa na kumpotosha mtu hivi kwamba akipata anadhani wengine hawastahili.

Wapo hata weusi, hasa wahamiaji, wasiotaka weusi waje kwa sababu wataibadili Amerika na hivyo basi kuondoa ile ‘fahari’ ya kuishi uzunguni. Uzuzu ulioje!

Ubinafsi unawaambia kuwa dola zao wanazotozwa kama ushuru hazifai kutumiwa kuboresha maisha ya watu wasio Wamarekani.

Sasa wamepata jembe – tingatinga hasa – la kufanya kazi hiyo, keti kitako ujionee shamba likilimwa.

Usiwe mnafiki ukawachukia Wamarekani; akilini mwako yumo mtu ambaye umetamani kupiga teke la makalioni ila huna nguvu au ujasiri wa kufanya hivyo.

Ukimpata wa kukupigia mtu huyo teke utamshangilia kimoyomoyo au hata umhimize waziwazi, fedheha ukifedheheka utaomba msamaha baadaye. Aibu! Komaa.

 

[email protected]

You can share this post!

Wachina 2 ndani kwa dai la kuuza chang’aa nchini

Mikakati ya Ruto kuingia Ikulu

adminleo