• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 PM
Bei ya ugali na mkate kupanda tena

Bei ya ugali na mkate kupanda tena

BARNABAS BII, GERALD BWISA na GEORGE SAYAGIE

GHARAMA ya maisha inatarajiwa kuongezeka kutokana na uwezekano wa kupanda kwa bei ya unga wa mahindi na ngano kutokana na uhaba wa nafaka hizo.

Bodi ya Kuhifadhi Chakula cha Dharura (SFR) jana ilitangaza kuongezeka kwa bei ya kila gunia la kilo 90 la mahindi linalonunuliwa kutoka kwenye maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kutoka Sh2,300 hadi Sh2,700.

Wakati huo huo, mavuno duni ya ngano katika Kaunti ya Narok, ambayo huzalisha zaidi ya nusu ya mazao yanayohitajika nchini, yatachangia kupanda kwa bei ya mkate na vyakula vingine vinavyotokana na ngano.

Makampuni ya kibinafsi ya kusaga mahindi yamesema uhaba huo utachangia kupanda kwa bei ya unga.

“Kazi yetu imekuwa chini sana kwa muda wa wiki mbili zilizopita. Hali hiyo imetulazimu kusimamisha shughuli hadi tupate mahindi ya kutosha ya kusaga,” akasema mmiliki ya kampuni ya kusaga mahindi mjini Eldoret, Kipngetich Mutai.

Mwenyekiti wa SFR, Dkt Noah Wekesa alisema kupanda kwa bei ya mahindi kumesababishwa na uhaba wa mazao hayo hata baada ya uagizaji kutoka mataifa wanachama wa EAC.

“Magunia milioni mbili yaliyoagizwa yatasambazwa kwa kampuni za kusaga mahindi ambazo zimesajiliwa. Tunatarajia kwamba kampuni hizi zitapunguza bei ya unga hadi kiwango ambacho wateja wanaweza kukimudu,” akasema Dkt Wekesa.

Taifa Leo iligundua kwamba bei ya pakiti ya kilo mbili ya unga imepanda kutoka Sh90 hadi kati ya Sh115 na Sh120 katika muda wa miezi miwili iliyopita.

Kupungua kwa mavuno ya ngano nako kunatokana na mvua nyingi iliyoshuhudiwa mwezi Aprili na Mei wakati ambapo mmea wa ngano hunawiri na hauhitaji maji mengi. Ndege pia walivamia ngano mwezi Juni na Julai na kuchangia upungufu zaidi.

Kulingana na baadhi ya wakulima wa ngano sababu hizo mbili zimechangia kupungua kwa mavuno kwa zaidi ya nusu ya hali ya kawaida.

Mkurugenzi wa Kilimo katika Kaunti ya Narok, Ben Kimetto alisema mavuno ya 2018 yalipungua kwa magunia milioni 1.2 kutokana na ukame wa muda mrefu hasa baada ya msimu wa upanzi.

You can share this post!

Walioegemea kwa Ruto sasa waapa kuletea ODM ushindi

Wapwani wakae ange upepo mkali ukitarajiwa wiki hii

adminleo