• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Ukarabati Bandari ya Kisumu waumiza wengi kibiashara

Ukarabati Bandari ya Kisumu waumiza wengi kibiashara

Na WAANDISHI WETU

MAELFU ya wafanyabiashara katika Kaunti ya Kisumu wanakadiria hasara kubwa baada ya majengo na vibanda vyao kubomolewa.

Ubomozi huo ulifanywa na serikali kuu katika juhudi za kukarabati Bandari ya Kisumu.

Ingawa mradi huo ni miongoni mwa ile inayochukuliwa kama minofu iliyotokana na handsheki ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, wakazi wa eneo hilo lililo ngome ya Bw Odinga kisiasa sasa wameachwa mataani.

Mradi huo umesifiwa kwamba utageuza Kisumu kuwa kitovu cha kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki kupitia kwa usafirishaji mizigo kwenye Ziwa Victoria.

Ripoti zinasema kuna wafanyabiashara wasiopungua 3,000 ambao wameathirika na bomoa bomoa ambayo inaendelea katika eneo hilo, wakiwemo wanasiasa.

Aliyekuwa Mbunge wa Gem, Bw Jakoyo Midiwo ambaye mkahawa wake ulibomolewa, jana alisema alipewa notisi ya siku 90 kuhama ambayo ilifaa kukamilika Oktoba 12 lakini akafurushwa siku 34 pekee baada ya kupokea notisi hiyo.

“Hii si haki. Nilikuwa nimeajiri watu zaidi ya 50 ambao maisha yao sasa yameathirika. Ombi langu kutaka Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Railways, Bw Odinga na Gavana Anyang’ Ngong’o waingilie kati halikuzaa matunda,” akasema Bw Midiwo.

Naibu Gavana wa Kisumu, Bw Mathews Owili alidai serikali ya kaunti imeanza kuwapa watu walioathirika sehemu mpya za kufanyia biashara zao.

“Tunasikitishwa na hasara iliyotokea lakini haya mambo yanafanyika kwa kasi mno. Kuna hali ya dharura kwa hivyo pia sisi tunatafuta jinsi ya kuwapa wote walioathirika sehemu mpya za kufanyia biashara zao ili kupunguza athari zinazotokana na shughuli hii nzima,” akasema.

Hata hivyo, alisisitiza watu wote waliokuwa katika ardhi za Kenya Railways na Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) watahamishwa.

Kulingana naye, baadhi ya wafanyabiashara wadogo wameanza kujengewa vibanda karibu na uwanja wa Jomo Kenyatta na katika ufuo wa Dunga.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Kitaifa la Biashara na Viwanda (KNCCI), Bw Israel Agina alisema ingawa ukarabati wa bandari ni muhimu, inapaswa wahusika waendeshe shughuli hiyo wakizingatia maisha ya binadamu.

“Tunafurahi na tumepokea maendeleo hayo kwa moyo mkunjufu lakini haistahili yalete masononeko kwa wakazi,” akasema Bw Agina.

Baadhi ya wafanyabiashara waliofurushwa wamesema sasa hawana budi ila kutafuta njia nyingine za kujikimu kimaisha, wakitumai watarudia hali yao ya awali angalau kabla watoto waanze kurudi shuleni mwezi ujao wakiwa na mahitaji chungu nzima.

Kuna wale ambao wateja sasa huwaita kuwahudumia nyumbani kama vile vinyozi na wasusi, huku wengine wakiamua kufanya biashara zao chini ya miti kama vile waliomiliki mikahawa midogo.

Bi Tabitha Ougo, ambaye ni mfanyabiashara aliyepoteza mkahawa, saluni na kinyozi katika eneo la Winmart ameamua kuendeleza huduma zake za uuzaji vyakula katika lango la Chuo Kikuu cha Maseno kilicho mjini.

Ripoti ya Justus Ochieng’, Victor Raballa, Rushdie Oudia na Lydia Ngugi

You can share this post!

Wapwani wakae ange upepo mkali ukitarajiwa wiki hii

Utahesabiwa utakapokuwa usiku wa Agosti 24 – Serikali

adminleo