Habari Mseto

Kaunti yatakiwa kubuni sera ya kupunguza chokoraa jijini

August 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA COLLINS OMULO

KAUNTI ya Nairobi imetakiwa kuunda sera kuhusu njia ya kuwarekebisha tabia watoto wa kurandaranda mitaani maarufu kama chokoraa ambao wanazidi kuvamia na kukita kambi katikati mwa mji.

Madiwani wa bunge la Kaunti ya Nairobi wametaka utawala wa Gavana Mike Sonko kuibuka na sera hizo ili kudhibiti idadi watoto hao ambao wamechangia ukosefu wa usalama mjini.

Diwani mteule Margaret Mbote kupitia hoja aliyowasilisha bungeni alikiri kufahamu jitihada za kaunti kuwafurusha chokora katikati mwa jiji ila akasema shughuli hiyo inafaa kuendeshwa kupitia utaratibu maalum.

“Katika muda wa miaka chache iliyopita, uwepo wa chokora jijini Narobi umekuwa tatizo linaloendelea kushuhudiwa na hili limeathiri biashara nyingi,” akasema Bi Mbote.

Aidha alidai kwamba chokora hutumiwa na mtandao wa walanguzi wa dawa za kulevya wanaozisafirisha kutoka eneo moja hadi jingine.

Vilevile alidai chokora hao wamebuni njia za kilaghai za kupata pesa kutoka kwa watu, baadhi wakijifanya ombaomba wanaohitaji fedha kutibu maradhi hatari ilhali ukweli ni kwamba hata hawaugui magonjwa hayo.

“Inasikitisha kuwa baadhi ya walanguzi hutumia chokora kuendesha biashara za dawa za kulevya na kutatiza vita dhidi ya mihadarati,” akaongeza Bi Mbote.

Mwaka jana, kaunti iliwaokoa zaidi ya watoto 700 wa kurandaranda mitaani na kuwapeleka katika makao ya watoto ya Makadara, Kayole, Shauri Moyo na Joseph Kang’ethe.