Habari

Kafyu nchi yote usiku wa sensa

August 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na WAANDISHI WETU

WAKENYA watatakiwa kukaa nyumbani kwao kuanzia saa kumi na moja jioni Jumamosi hii hadi Jumapili ili wahesabiwe.

“Hakutakuwa na kesha ama sherehe za kibinafsi zitakazoruhusiwa siku ya sensa. Hakuna baa itakayofanya kazi. Watu hawataruhusiwa kutembea usiku. Kila mtu atahitajika kuwa nyumbani kwake kufikia saa kumi na moja jioni hapo Jumamosi. Polisi watakuwa macho kuhakikisha watu wako manyumbani,” akasema Kamishna wa Kanda ya Kati, Wilfred Nyagwanga.

Kauli yake inasisitiza agizo la maafisa wa serikali wakiongozwa na Waziri wa Usalama wa Nchi Fred Matiang’i, makamishna wa kaunti na magavana.

Kulingana na maafisa hao, makanisa, sherehe za kibinafsi, mabaa na sehemu nyingine za kijamii hazitaruhusiwa kufunguliwa.

Wasafiri ambao hawatakuwa wamehesabiwa nao hawataruhusiwa kuendelea na safari zao.

Jumatano, Dkt Matiang’i aliagiza baa zote nchini kufungwa Jumamosi saa kumi na moja jioni, na akawaagiza polisi na machifu kuhakikisha agizo hilo linatakelezwa.

Lakini kulingana na wanasheria, agizo hilo pamoja na mengine ya makamishna wa kaunti ni ukiukaji wa madaraka yao na upuuzaji wa Katiba.

Kulingana na Katiba, jukumu la kuagiza kufungwa kwa mabaa ni la Idara za Afya kwenye kaunti ama Bodi za Leseni za Pombe ambazo ziko chini ya serikali za kaunti.

Katiba pia imetoa uhuru wa kujumuika kijamii bila vikwazo.

Kulingana na Wakili Lempaa Suyanka, polisi hawawezi kumfungulia yeyote mashtaka kwa kupatikana kwenye baa ama kanisani siku hiyo iwapo hajakiuka sheria zilizopo kama vile Sheria za Mututho zinazohusu pombe.

“Hakuna sheria ambayo polisi wanaweza kutumia kumshtaki mtu kwa kufungua ama kuwa kwenye baa siku hiyo,” akasema Bw Lempaa.

Shughuli ya kuhesabu watu itaanza Jumamosi jioni na kuendelea kwa siku saba hadi Agosti 31, lakini siku zitakazotiliwa mkazo zaidi ni Agosti 24 na 25.

Wakenya wote watahitajika kuwa manyumbani mapema wakisubiri kuhesabiwa,” akasema Dkt Matiang’ia akiwa Embu.

Alisema maafisa wa polisi walio likizoni wameitwa ili kusaidia katika kuimarisha usalama.

Katika Kaunti ya Makueni, Kamishna Mohammed Maalim alisema wasafiri watahesabiwa katika miji ya Mtito Andei, Emali na Salama kwenye barabara ya Nairobi-Mombasa kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari zao.

Bw Maalim alisema maafisa wa kuhesabu watu wakiandamana na polisi wataweka vizuizi kwenye maeneo hayo matatu kuhakikisha kila msafiri amehesabiwa.

“Madereva watasimamishwa katika kila moja ya vizuizi hivyo kukaguliwa iwapo wamehesabiwa. Kila msafiri atahitajika kujaza fomu kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari,” akasema Bw Maalim.

Naye Gavana Kivutha Kibwana aliagiza baa zote zifungwe kwa saa 24 kuanzia Jumamosi saa kumi na moja.

Katika Kaunti ya Nakuru, Gavana Lee Kinyanjui aliwaomba wenyeji kukaa manyumbani siku ya sensa.

Pia aliwaomba wazaliwa wa kaunti hiyo wanaoishi nje kurudi kuhesabiwa maeneo yao ya kuzaliwa.

Gavana Alfred Mutua naye amepiga marufuku kufunguliwa kwa kila aina ya biashara Kaunti ya Machakos.

Kurudi nyumbani

Katika Kaunti ya Nyandarua, wanasiasa, wahubiri na wafanyibiashara wameungana kuhimiza wazaliwa wa kaunti hiyo kukubali kurudi makwao ili kuhesabiwa huko.

Wahubiri waliendeleza kampeni hiyo wakisema kuwa hata Biblia inahitaji watu kuhesabiwa mahali walikozaliwa.

Katika Kaunti ya Baringo, wanasiasa wamehimiza kuimarishwa kwa usalama katika maeneo ya Baringo Kusini na Kaskazini ili kufanikisha zoezi hilo.

Viongozi hao walisema wana hofu kuwa majangili wanaweza kutumia shughuli hiyo kushambulia wakazi hasa katika maeneo ya Chemoe, Yatya, Kagir, Ng’aratuko, Chepkesin, Kamwetio, Kaborion, Kapturo, Kinyach na Loruk.

Jijini Mombasa, Kamanda wa Polisi Gilbert Kitiyo aliwaambia wakazi wasiwe na hofu kuhusu usalama wao usiku wa kuhesabiwa.

“Nafahamu wengi wenu mna hofu sana kwa sababu shughuli hiyo inafanyika usiku. Lakini usalama umeimarishwa kwani watakaokuwa wanaendeleza shughuli hiyo watakuwa wamevalia sare ambazo zimechorwa nembo ya serikali na wataandamana na maafisa wa usalama na wazee wa mtaa,” akasema Bw Kitiyo.

Nako Turkana, Mbunge wa Turkana Kaskazini Christopher Nakuleu amelitaka Shirika la Takwimu nchini (KNBS) kuwafadhili walioajiriwa kuendesha shughuli za sensa ili kuhakikisha kuwa wakazi wote wanahesabiwa.

Akitoa mfano wa eneo bunge lake, Bw Nakuleu alisema kuwa makarani wa kuhesabu watu kaunti ndogo za Kibish na Turkana Kaskazini hawajapewa nauli ya kutosha na chakula.

 

Ripoti za George Munene, Regina Kinogu, Pius Maundu, Phyllis Musasia, Waikwa Maina, Sammy Lutta, Florah Koech, Cece Siago na Farhiya Hussein