• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:10 PM
Maporomoko ya ardhi yasababisha maafa China

Maporomoko ya ardhi yasababisha maafa China

Na AFP

BEIJING, China

WATU tisa wamefariki na wengine 35 bado hawajulikani waliko kufuatia msururu wa maporomoko ya ardhi yaliyoshuhudiwa katika mkoa wa Sichuan ulioko Kusini Magharibi mwa China, maafisa wa utawala wamesema.

Mhudumu mmoja wa shirika la uokoaji, mwenye umri wa miaka 33, ni miongoni mwa waliofariki katika mafuriko yaliyoangusha gari lao walipokuwa wakienda kuwasaidia watu walioathirika na maporomoko ya ardhi katika Kaunti ya Wenchuan, maafisa hao wakasema.

Maporomoko hayo na mafuriko yanatokana na mvua kubwa inayonyesha katika mkoa huo wa Sichuan na maeneo ya karibu.

Shirika la habari la serikali, Xinhua limesema mhudumu mwingine wa idara ya zimamoto alikuwa akipokea matibabu ya dharura, lilinukuu wasimamizi wa shirika la uokoaji la Sichuan.

Watu wengine sita wameripotiwa kujeruhiwa huku zaidi ya watu 100,000 wakihamishwa kutoka Wenchuan hasa maeneo ya milima ya Aba Tibetan na Oiang.

Mvua kubwa na maporomoko hayo ya ardhi yalivuruga mfumo wa usambazaji maji na umeme kwa maelfu ya makazi, kando na kuharibu madaraja na barabara zinazoelekea jiji la Chengdu, ambalo ndilo mji mkuu wa mkoa wa Sichuan.

Maafisa walisema kuwa wametuma mabasi 20 na helikopta mbili kuwaokoa watalii katika eneo hilo ambalo hutembelewa na watalii wengi.

You can share this post!

Museveni na Kagame waridhiana

‘Sensa kuwanyima wapenzi wa kabumbu mechi ya Arsenal...

adminleo