• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kenya kuunda Baraza la Kiswahili mswada ukifaulu kuidhinishwa

Kenya kuunda Baraza la Kiswahili mswada ukifaulu kuidhinishwa

Na ANGELINE OCHIENG’

KENYA itakuwa taifa la pili Afrika Mashariki na Kati kubuni Baraza la Kiswahili iwapo mswada ambao unaandaliwa na wasomi wa lugha hiyo utaidhinishwa na bunge.

Mswada huo ambao uliwasilishwa kwa wasomi wa lugha hiyo kwenye warsha moja mjini Kisumu jana, bado upo kwenye hatua za mwanzo za utayarishaji wake.

Iwapo utapitishwa bungeni, Kenya itakuwa kwenye kikoa kimoja na Tanzania ambayo huendesha shughuli nyingi za serikali kwa lugha ya Kiswahili na inajivunia uwepo wa Baraza Kuu la lugha hiyo.

Kulingana na msomi wa Kiswahili na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Laikipia, Dkt Sheila Wandera, kubuniwa kwa baraza hilo ni ndoto ambayo ikitimia basi itaikweza hadhi Kiswahili na kukifanya kithaminiwe hata zaidi.

“Baada ya kubuniwa kwa baraza la Kiswahili, tutakuwa na jukwaa la kutatua tofauti kuhusu matumizi ya misamiati na nomino zenye utata. Ingawa Kiswahili kilipandishwa hadhi kuwa lugha rasmi na ya kitaifa, baraza litalainisha matumizi yake nchini,” akasema Dkt Wandera.

Kwa muda mrefu Kiswahili hakijakuwa kikizingitiwa sana kama lugha ya taifa kwa kuwa hafla nyingi za serikali bado huendeshwa kwa Kiingereza.

Kando na kuwa na baraza la Kiswahili, Tanzania imekuwa mfano bora kwa mataifa ya Afrika Mashariki kwa kuthamini lugha hii na kuitumia mara nyingi kwa shughuli rasmi za serikali.

Matumizi ya Kiswahili wiki jana yalipigwa jeki baada ya mataifa wanachama wa Muungano wa Kiuchumi kwa Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuikumbatia kama lugha ya nne ya kutumika wakati wa vikao vyake.

Mchakato

Vilevile, mataifa ya Lesotho na Malawi ni kati ya mengine 16 Kusini mwa Afrika ambayo yapo kwenye mchakato wa mwisho wa kuanzisha ufundishaji wa Kiswahili kama somo kwenye shule zao za msingi, upili na hata vyuo vikuu.

Raia kutoka Mabara ya Asia, Marekani na Ulaya nao wameanza kukisoma Kiswahili huku waliokamilisha masomo yao wakiwa mstari wa mbele kutafsiri vitabu vilivyoandikwa kwa Kingereza hadi Kiswahili.

Pia kuna uwezekano kwamba Kiswahili huenda kikatajwa kati ya lugha saba maarufu duniani kwa muda wa miezi michache ijayo.

You can share this post!

Maraga ahimiza Wakenya kuwafichua maafisa fisadi

Tamasha ya kumuenzi De’ Mathew kuandaliwa leo Ijumaa

adminleo