TAHARIRI: Tujitokeze sote tushiriki sensa
Na MHARIRI
HATIMAYE siku ya sensa imefika, ikiwa shughuli muhimu kwa kila taifa.
Hii ni shughuli inayofanyika kila baada ya miaka 10, kumaanisha itafanywa tena mwaka wa 2029.
Maandalizi yamekamilika na serikali imewataka raia wote kutulia nyumbani na kuwakaribisha maafisa wa kuhesabu watu watekeleze shughuli hiyo.
Hivi ndivyo kila mtu anavyopaswa kufanya na tunahimiza Wakenya kutupilia mbali malalamishi na tofauti zao za kisiasa ili kushiriki kikamilifu kwa manufaa ya nchi yao.
Ni kutokana na kujua idadi ya raia wake ambapo serikali inaweza kuweka mipango ya maendeleo.
Takwimu ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi, na kwa hivyo tunaomba kila Mkenya kuhakikisha amehesabiwa.
Kukosa kuhesabiwa ni sawa na kukataa uraia wa Kenya. Kuna waliotisha kuvuruga shughuli hiyo na pengine hawajui kwamba hawawezi kushindana na serikali.
Wanaodai kuwa walibaguliwa wakati wa kuajiri maafisa wa kutekeleza shughuli hiyo wanafaa kukoma hasira zao kwa sasa. Hasira daima ni hasara na hazitendi haki kwa Mungu.
Maafisa wa kuhesabu watu nao wanapaswa kuheshima kiapo walichokula cha kuweka siri habari zote watakazopata kutoka kwa raia.
Aidha, serikali inapaswa kutimiza ahadi yake ya kuhakikishia Wakenya usalama. Itakuwa vibaya kwa watu wakiwemo maafisa wanaotekeleza shughuli hiyo kushambuliwa kama ilivyofanyika Kaunti ya Wajir mnamo Alhamisi.
Usalama wa raia na maafisa utahakikisha habari sahihi zitapatikana na ukikosekana, itamaanisha habari zitakuwa na dosari.
Serikali pia ihakikishe kwamba wanasiasa hawatateka shughuli hiyo kwa tamaa yao.
Hesabu kamili ya watu katika eneo fulani huwezesha serikali kutimizia wananchi wa eneo hilo maendeleo bila ubaguzi ni sio wanasiasa ambao kazi yao ni kutumia raia kama vyombo vya kuwaweka mamlakani na kisha kuwasahau.
Huu ni wakati wa kila Mkenya kujitokeza na kujivunia kuwa Mkenya kwa kuhesabiwa na sio kufurahisha wanasiasa kwa kufanya wanavyotaka. Hivyo basi, tunawahimiza Wakenya kutulia popote walipo kuhesabiwa badala ya kufuata miito ya wanasiasa na kutumia gharama nyingi kusafiri kwenda mbali.
Ni matumaini yetu pia kwamba serikali itatumia takwimu itakazopata kulainisha shughuli zake hasa kufanikisha ugatuzi zaidi.