Magavana njiapanda kuhusu miswada miwili
Na GITONGA MARETE na CHARLES WASONGA
MAGAVANA sasa wako njia-panda kuhusu iwapo waunge mkono kura ya maamuzi inayopendekezwa ya Punguza Mizigo au wakuu wa vyama vyao, wanaounga mchakato wa jopo la Maridhiano (BBI).
Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa ODM Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wa Wiper wamepinga mswada wa Punguza Mizigo unaopendekeza kuongezwa kwa mgao wa fedha katika kaunti, hatua inayoungwa mkono na magavana wote 47.
Idadi kubwa ya magavana hao walichaguliwa kwa udhamini wa vyama vya Jubilee, ODM na Wiper.
Mswada wa Punguza Mizigo uliotayarishwa na Chama cha Thirdway Alliance kinachoongozwa cha Ekuru Aukot pia unapendekeza kupunguzwa na idadi ya wabunge na maseneta kutoka 416 hadi 147.
Lakini BBI inaonekana kulenga kuongeza gharama katika ngazi ya kitaifa kwa kubuni nyadhifa zaidi za uongozi kama waziri mkuu na manaibu wawili, hali ambayo itapunguza mgao wa fedha kwa kaunti.
Lakini Gavana wa Meru Kiraitu Murungi sasa ameonyesha dalili za kupendelea Mswada wa Punguza Mizigo alipoeleza kuwa ataunga mkono mpango unaolenga kuongeza ufadhili kwa serikali za kaunti.
“Hata kama itakuwa Punguza Mizigo au BBI kile muhimu kwa magavana ni pesa zaidi zielekezwe kwa serikali za kaunti,” akasema.
Kauli ya Bw Kiraitu ambaye ni mfuasi mkubwa wa Rais Kenyatta inaashiria kuwa Rais anapaswa kutarajia upinzani mkali kutoka kwa magavana kuhusiana na shinikizo zake za kura ya maamuzi kupitia mchakato wa BBI.
“Tunapewa asilimia 20 pekee ya mapato ya kitaifa ilhali ni sisi tunatekeleza asilimia 80 ya kazi. Hii ina maana kuwa pesa nyingi inasalia katika serikali ya kitaifa kutekeleza asilimia 20 pekee ya kazi. Hii sio haki. Serikali za kaunti zinapasa kupewa asilimia 80 ya mapato ya kitaifa,” akasema.
Gavana Murungi alikuwa akiongea katika Shule ya Msingi ya Gitoro Alhamisi wakati wa mkutano wa kutoa uhamasishaji kwa wadau kuhusu Ruwaza ya Maendeleo ya Kaunti ya Meru hadi 2040. Ruwaza hii inaelezea miradi ya maendeleo itakayotekelezwa katika kaunti hiyo kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.
Mvutano
Kumekuwa na uhusiano usio mzuri baina ya Rais Kenyatta na Magavana kufuatia mvutano unaotokota kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato (DoRB).
Magavana wamekuwa wakiikashifu Serikali ya Kitaifa kwa kula njama na Bunge la Kitaifa kuzinyima serikali za kaunti mgao mwafaka wa fedha katika mwaka huu wa kifedha (2019/2020).
Wabunge wanapendekeza kaunti zigawiwe Sh316 bilioni lakini Maseneta wanataka mgao wa Sh335 bilioni, pendekezo linaloungwa mkono na magavana.
Kila Bunge limekataa kulegeza msimamo wake hali ambayo imechangia mzozo wa sasa ambao umesabisha serikali za kaunti kukosa kuwalipa wafanyakazi mishahara ya mwezi Julai.
Na Rais Kenyatta amejitokeza wazi akisema kuwa serikali haina pesa za kuziongezea serikali za kaunti, akizihimiza kuhakikisha kuwa zimejiongezea mapato kwa kuimarisha viwango vyao vya ukusanyaji ushuru.
“Serikali haina pesa za kuwaongezea magavana. Ikiwa nyinyi wabunge mnataka kuwaongezea basi mkubali kupunguza mishahara yenu ili pesa za ziada zipatikane,” Rais akasema juzi alipohudhuria mazishi ya mamake aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth.