• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Kongamano lajadili maswala muhimu ya kuinua wanawake

Kongamano lajadili maswala muhimu ya kuinua wanawake

Na LAWRENCE ONGARO

WANAWAKE nchini wanataka waheshimiwe na kupata nyadhifa muhimu za uongozi angalau kwa hadi asilimia 50.

Zaidi ya wanawake 100 kutoka kaunti 11 kote nchini walikongamana mjini Thika ili kujadiliana maswala ya kutambuliwa katika uongozi wa nchi hii.

Mkurugenzi wa shirika la Groots Kenya, Bi Fridah Githuku, alisema huu ndio wakati wa wanawake kujitokeza wazi kutambulika katika uongozi.

Alisema madhumuni hasa ya kongamano hilo la wanawake yalikuwa kutathmini ni yapi serikali imetekeleza kuwainua wanawake kwa muda wa miaka 25 tangu mkutano mkuu wa kimataifa wa Beijing nchini Uchina.

Mkurugenzi wa Shirika la Groots Kenya Bi Fridah Githuku akihutubia wanahabari Agosti 23, 2019, mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema mwaka 2020 Umoja wa Mataifa (UN) utasherehekea miaka 25 tangu mkutano mkuu wa wanawake ulipofanyika Beijing, Uchina.

Kuhusu kuunga mkono kura ya maamuzi ambayo huenda ikaandaliwa, alieleza kuwa hawako tayari kwa sasa kujianika wazi kusema wako upande upi, lakini kati ya mirengo miwili ya Punguza Mizigo na BBI, wowote ulio na mvutio wa kuweka ugavi wa mamlaka kwa asilimia 50 kwa 50 kwa jinsia mbili ina maana watakuwa tayari kumshabikia kama wanawake.

“Kwa muda mrefu sisi wanawake tumekuwa tukitupiwa lawama kuwa hatujitumi katika kutafuta uongozi, lakini ukweli wa mambo ni kwamba wengi hukosa fedha za kuwapeleka mbele,” alifafanua Bi Githuku.

Alisema katika kiwango cha Kaunti uongozi wa wanawake hauonekani kabisa kwa sababu ni wachache sana wanapata nyadhifa za juu.

Alipendekeza serikali ijayo iwape wanawake nyadhifa za juu hata ya Naibu Rais na pia wagombanie kiti cha Rais wa nchi.

Majadiliano

Bi Winrose Nyaguthii Mwangi, alisema wao kama wanawake wako tayari kujadiliana matakwa yao ili waingie uongozini kwa wingi.

“Mara hii katika uchaguzi tutafanya juhudi kuona ya kwamba tunaingia uongozini kwa wingi ili tutambulike. Kile tunahitaji ni rasilimali za kujiendeleza,” alisema Bi Mwangi.

Alieleza kuwa wanawake kutoka mashinani wana majukumu mengi na ni vyema kutambuliwa uongozini.

Naye Bi Wairimu Kanyiri kutoka Kaunti ya Nakuru, alisema wanawake mashinani ni wakulima wenye bidii.

“Serikali inastahili kuwapa fedha za mikopo ili kuendeleza kilimo vijijini. Wao ndio wakuzaji wa viazi, karoti, na ndio wafugaji na kwa hivyo wanastahili pia kutambulika katika viwango vya juu,” alisema Bi Kanyiri.

Bi Susan Kioko wa kutoka Kaunti ya Kilifi, Pwani, alisema serikali bado haijatambua wanawake kikamilifu; hasa walio vijijini.

“Sisi wanawake tunataka kutambuliwa kutokana na juhudi zetu tunazofanya mashinani. Hii itafanikiwa tu iwapo kuna nia njema ya ushirikiano,” alisema Bi Kioko.

You can share this post!

Rasharasha na kijibaridi kikali katika maeneo mengi kipindi...

Shughuli zatatizika Knut kutokana na ukosefu wa fedha

adminleo