• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
Rais aongoza viongozi wengine serikalini kumuaga mwanamuziki De’ Mathew

Rais aongoza viongozi wengine serikalini kumuaga mwanamuziki De’ Mathew

Na WANDERI KAMAU

MAELFU ya waombolezaji Jumamosi walimuaga kishujaa mwanamuziki maarufu wa nyimbo za Kikuyu John De’ Mathew katika Shule ya Msingi ya Githambia, eneobunge la Gatanga, Kaunti ya Murang’a.

Miongoni mwa wale waliofika kwenye mazishi hayo ni Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, mawaziri Joe Mucheru (Habari, Mawasiliano na Teknolojia), Mwangi Kiunjuri (Kilimo), James Macharia (Uchukuzi), Amina Mohamed (Michezo), mwanasiasa Peter Kenneth miongoni mwa wengine.

Mashabiki wake walianza kuwasili katika Chumba cha Kuhifadhi Maiti cha Chuo Kikuu cha Kenyatta saa 12 alfajiri ili kupata nafasi ya kuutazama mwili wake.

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo alikuwa na wakati mgumu kuudhibiti umati huo, baada ya watu hao kujaribu kuingia ndani kwa nguvu.

Bw Kabogo alilazimika kupanda juu ya lango kuu kuwahakikishia kuwa kila mmoja atafanikiwa kuutazama.

Ilichukua muda wa dakika 30 kuwatuliza ili kuanza kuutazama mwili hio.

Saa mbili baadaye, mwili huo ulielekezwa nyumbani kwake kwa mazishi.

Wazungumzaji mbalimbali walimsifu kwa kujitolea na mchango wake mkubwa aliotoa katika ukuzaji wa muziki, hasa eneo la Mlima Kenya.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto walisema kwamba De’ Mathew wakati wa uhai wake aliwasaidia sana kwenye kampeni zao mnamo 2013 na 2017 na wakati walikabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

“Alitusaidia kwenye kampeni zetu kwani tulizuru sehemu mbalimbali nchini tukitafuta kura,” akasema Bw Kenyatta.

Walisema kuwa ni kutokana na nyimbo zake ambapo waliweza kuwafikia Wakenya wengi zaidi.

Wake zake wawili, Bi Sarafina Wairimu na Bi Caroline Waithera walimsifu kama rafiki anbaye hawatamsahau.

Watoto wake vilevile walimtaja kama baba aliyejitolea kuwalea, kwa kuhakikisha kuwa hawakukosa chochote walichohitaji.

Ujumbe wao ulikuwa: ‘Ahsante kwa kutuonyesha maana halisi ya kuwa mfano mwema kwa jamii na mwanamuziki bora’.

Huzuni

Kwa wakati mmoja, jamaa zake walishindwa kusoma jumbe hizo kwa kuzidiwa na hisia, hali iliyomlazimu mshirikishi wa hafla hiyo Bw Njogu Njoroge kuwaomba watu wengine kuzisoma.

Wanamuziki mbalimbali pia walimsifu kwa kuwa nguzo kwenye uzinduzi wa Chama cha Ushirika cha Tamco, kinachowashirikisha wanamuziki wote kutoka ukanda huo.

Wanamuziki Ben Githae, Loise Kim, Peter Kigia kati ya wengine ambao ni viongozi wa chama hicno walisema kwamba ni kupitia shinikizo za marehemu ambapo walikusanyika na kukibuni ili kuimarisha maslahi ya wanamuziki.

Marehemu alifariki Jumapili iliyopita kwenye ajali ya barabarani katika eneo la Blue Post, karibu na mji wa Thika. Alifariki akiwa na umri wa miaka 52.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Masaibu tele kwa familia ambayo...

Matiang’i na Kibicho mwiba kwa Naibu Rais

adminleo