Mahakama yazima mpango wa kaunti kutwaa ardhi ya umma
TOM MATOKE na WYCLIFF KIPSANG
SERIKALI ya Kaunti ya Nandi imepata pigo baada ya Mahakama Kuu kusitisha nia ya utawala wa Gavana Stephen Sang’ kutwaa ardhi yote ya umma inayomilikiwa na wafanyabiashara kwenye kaunti hiyo.
Korti hiyo iliagiza utawala wa kaunti kutotwaa ardhi hizo, uamuzi ambao umekumbatiwa kwa furaha kuu na wafanyabiashara hao ambao wanadai kuzimiliki kihalali.
Uamuzi huo ulitolewa baada ya serikali ya kaunti kuwaamrisha wafanyabiashara zaidi ya 100 kutoa stakabadhi za umiliki wa ardhi za umma na kuonyesha jinsi walivyotwaa vipande vyao vya ardhi.
Jaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi, M Odeny mjini Eldoret, alitoa amri hiyo ambayo sasa inazuia kaunti kutovuruga mipango ya kibiashara ya wamiliki wa ploti hizo.
“Ombi la wafanyabiashara lina uzito na ni la dharura,” uamuzi ulieleza.
Wafanyabiashara walipinga mpango wa serikali hiyo kuwaondoa kwenye ardhi walizonunua kati ya 1963 na 2019, wakisema kaunti ina nia ya kuwavuruga wawekezaji kutokana na misimamo yao kuhusu siasa za Nandi.
Kamati kuu ya Kaunti ya Nandi mnamo Julai 6, 2019 iliafikiana kwamba wamiliki wote wa ardhi wawasilishe stakabadhi muhimu kabla ya makataa ya siku 21 ikidai kwamba ploti hizo zilipatikana kwa njia haramu.