Hamdok achukua hatua za kutaka kuiondoa Sudan kwenye orodha mbaya
Na MASHIRIKA
SUDAN huenda ikaanza kupokea uwekezaji kutoka nchi za kigeni pamoja na ufadhili wa kifedha huku Waziri Mkuu mpya nchini humo Abdalla Hamdok, akichukua hatua za kuhakikisha taifa lake kunaondolewa kwenye orodha ya Washington kuhusu mataifa yanayofadhili ugaidi.
Hamdok alisema amezungumza na maafisa wa Amerika kuhusu kuiondoa Sudan kama mojawapo ya mataifa yaliyoorodheshwa kama wafadhili wakuu wa shughuli za kigaidi.
“Huku Sudan ikianza ukurasa mpya, kuondoka katika orodha ya Amerika kuhusu ufadhili wa ugaidi ndilo jambo ‘kuu’ zaidi tunaloweza kufanyia taifa hili,” Hamdok alieleza vyombo vya habari Jumapili, akisema kwamba taifa la Sudan si tishio kwa yeyote ulimwenguni.
Haya yamejiri siku chache tu baada ya kiongozi huyo kuchukua usukani wa serikali ya mpito nchini humo inayokumbwa na utata kuhusu utawala wa uraia na jeshi.
Uteuzi wake rasmi wiki iliyopita ulifuatia maandamano makubwa yaliyosababisha kung’atuliwa mamlakani kijeshi mnamo Aprili, kwa Rais Omar al-Bashir aliyetawala kimabavu kwa muda mrefu.
Baraza kuu linalojumuisha raia sita na wanajeshi watano linatazamiwa kutawala nchi hiyo kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu hadi uchaguzi utakapofanyika.
Kulingana na Hamdok, hatua ya kuiondoa Sudan kwenye orodha hiyo itafungua milango kwa uwekezaji wa kigeni na kuruhusu taifa hilo kupokea msaada unaohitajika zaidi wa Hazina ya Kimataifa kuhusu Fedha na ufadhili wa Benki ya Ulimwengu.
Tangu 1993
Amerika iliiorodhesha Sudan kama taifa linalofadhili “ugaidi” mnamo 1993, na ikadumu katika hali hiyo katika utawala wote wa al-Bashir.
Kama mojawapo ya hatua za mwisho za utawala wa Obama, Amerika ilianza mchakato rasmi wa kuiondoa Sudan katika orodha hiyo mnamo Januari 2017, huku ikifutilia mbali vikwazo vya kibiashara na kiuchumi mnamo Oktoba.
‘Tunafahamu na kuelewa kwamba, kuna mchakato katika serikali pamoja na Congress,’ alisema Hamdok, akiongeza kuwa anatumai itafanyika hivi karibuni kwa kuwa “ina matokeo muhimu mno katika hali yetu.”
‘Kwa miaka 30 tulitengwa. Tulichukuliwa kama taifa lisilohitajika. Tunataka kueleza ulimwengu kwamba tunaondoka kwenye vikwazo, masuala ya adhabu na mambo hayo yote na kuwa Sudan inayorejea katika hali ya mataifa ya kawaida,” alisema.
Sudan ina deni la karibu Sh6.2 bilioni ambapo Hamdok alisema riba ya deni hilo ni Sh3.1 bilioni.Mkataba wa kugawana mamlaka kati ya viongozi wa maandamano na Baraza la Mpito la Kijeshi Sudan, (TMC) ulitiwa sahihi mapema mwezi huu.
Jeshi lilimfurusha al-Bashir mnamo Aprili kufuatia miezi kadha ya maandamano makubwa lakini waandamanaji waliendelea kufurika barabarani wakihofia jeshi huenda likakatalia mamlakani na kudai uhamishaji mara moja katika serikali ya kiraia.
Mkataba wa kugawana mamlaka kati ya viongozi wa maandamano na TMC ulitiwa sahihi mapema mwezi huu na kumaliza kipindi cha miezi kadha cha taharuki na ghasia za kisiasa.
Imetafsiriwa na Mary Wangari