Habari Mseto

Serikali yakanusha madai ya kufurusha wakazi Mau

August 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMUEL BAYA

SERIKALI imesisitiza kuwa hakuna shule wala taasisi za umma katika eneo la msitu wa Mau ambako inapanga kufurusha watu.

Awamu ya pili ya kuhifadhi msitu wa Mau Narok inatarajiwa kuathiri zaidi ya familia 10,000 ingawa serikali ilitangaza kwamba waathiriwa watapatiwa muda wa miezi miwili kabla ya kuondolewa.

Akiongea na waandishi wa habari afisini mwake, mwenyekiti wa jopo lililobuniwa kuhifadhi msitu huo Bw George Natembeya alisema kuwa matamshi ya baadhi ya viongozi wa bonde la ufa kwamba kuna shule na taasisi nyingine za serikali kuwa makosa makubwa na uongo.

Jumamosi iliyopita, viongozi kutoka Bonde la ufa walisema kuwa eneo ambalo serikali inapanga kufurusha watu katika msuto huo lina shule pamoja na wawakilishi watatu wa wadi.

“Eneo hilo la Mau liko na wawakilishi wa wadi watatu, shule kadhaa na kuna zaidi ya wanafunzi 10,000. Sasa wakati serikali ikibuni wadi, haikujua kwamba zilikuwa katika msitu,” akadai Seneta wa Elgeiyo Marakwet Bw Kipchumba Murkomen.

Lakini Bw Natembeya katika kikao na waaandishi wa habari alitaja matamshi hayo kama ya kueneza hisia kali kwa wenyeji ingawa hayana ukweli.

“Hii ni kuongeza tu hisia na kuonyesha serikali kana ambayo haijali maslahi ya wakenya na huo ni uongo. Hakuna shule yoyote huko, ni wanafunzi gani hao ambao sisi hatujawaona ila leo hii wanatangazwa kuwa huko. Pateni hili kutoka kwangu, mimi kama kamishna wa eneo hili, hakuna mwanafunzi hata mmoja huko,” akasema Bw Natembeya.

Alisema kuna haja ya viongozi na kushirikiana na serikali katika kutafuta sulushihiso la kudumu katika uhifadhi wa msitu huo wa Mau wala sio kubishana kila mara wakati uharidifu ukiendelea.

Aliongeza kwamba suala hilo halihusishi jamii za Wamaasai wala wakipsigs wala kabila lolote lengine.