• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
UNHCR yapinga hatua ya TZ kutimua wakimbizi wa Burundi

UNHCR yapinga hatua ya TZ kutimua wakimbizi wa Burundi

Na AFP

WAKIMBIZI 200,000 kutoka Burundi wamepewa makataa ya mwezi mmoja kuondoka Tanzania la sivyo watarejeshwa kwao kwa nguvu.

“Kwa sasa kuna amani nchini Burundi, kwa hivyo wakimbizi wote wanaoishi humu nchini wanatakiwa kurejea kwao kwa hiari kufikia Oktoba 1. Baada ya makataa hayo tutawarejesha kwao kwa nguvu iwe wanataka au la,” akasema waziri wa Masuala ya Ndani ya nchi, Kangi Lugola.

Raia hao wa Burundi walitoroka nchi yao kufuatia machafuko yaliyotokea mnamo 2015 wakati wa maandamano ya kupinga Rais Pierre Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.

Baada ya miezi mitatu, serikali iliandaa kura ya maamuzi na kubadili katiba kumwezesha Rais Nkurunziza kusalia mamlakani hadi 2034.

Wakimbizi hao wanaishi katika kambi za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli kusini-magharibi mwa mkoa wa Kigoma.

Mwaka jana, serikali ya Tanzania na Burundi ziliafikiana kuwa zitakuwa zinarejesha nyumbani wakimbizi 2,000 kila wiki.

Lakini Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) lilipuuza maafikiano hayo.

Shirika la UNCHR limeshikilia kuwa mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi, unapiga marufuku kurejesha kwa nguvu wakimbizi katika mataifa ambayo wametoroka.

Ijumaa iliyopita, Waziri Lugola na mwenzake wa Burundi Pascal Barandagiye walitembelea kambi ya wakimbizi ya Nduta ambapo alitangaza mpango wa kuwarejesha makwao.

Wakati wa ziara hiyo, waziri Lugola alisema serikali haitakubali mpango huo kutatizwa na mashirika ya kimataifa au wageni.

Serikali ya Burundi tayari imeshutumu UNCHR kwa kuwa kikwazo kwenye mchakato wa kuwarejesha nyumbani raia wake walioko katika nchi jirani ya Tanzania.

Barandagiye wiki iliyopita alisema kuwa shirika la UNHCR ndilo linatatiza mpango huo na ‘linalenga kuzua uhasama baina ya serikali za Tanzania na Burundi’.

“Shirika la UNCHR lilipoulizwa na serikali ya Burundi kwa nini wakimbizi wanaorejea nchini ni idadi ndogo, walijibu kuwa hao ndio serikali ya Tanzania iliyoweza kuwaorodhesha. Na serikali ya Tanzania ikiulizwa inasema kuwa serikali ya Burundi imependelea hivyo kwani haina uwezo wa kuwapokea. Hivyo tumegundua UNHCR inalenga kuzua uhasama baina ya serikali hizi mbili. Na ni kikwazo kwa mchakato wa kurejesha wakimbizi nchini.” akasema Barandagiye.

Baadhi ya wakimbizi wamepinga mpango wa kurejeshwa makwao huku wakisema kuwa watahatarisha maisha yao.

Kulingana na wakimbizi hao, serikali ya Nkurunziza ingali inaendeleza visa vya utekaji nyara na dhuluma.

“Watu wamekuwa wakitekwa nyara na kisha miili yao kupatikana imetupwa misituni. Mbona wanataka turejee nyumbani kuuawa?” akasema mmoja wa wakimbizi hao.

Msemaji wa UNHCR Dana Hughes alitaka Tanzania na Burundi kuheshimu mkataba wa kimataifa kuhusu hifadhi kwa wakimbizi.

You can share this post!

Atimuliwa kuishi na mume kwa kakake

Wavuvi hatarini kunyimwa kibali kwa kupuuza kanuni

adminleo