Jaji mkuu David Maraga afungua mahakama ya mjini Ruiru
Na LAWRENCE ONGARO
KUNA haja ya serikali kujenga Mahakama nyingi kote nchini ili kutosheleza maswala ya upatikanaji haki na huduma zingine muhimu za kisheria, amesema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu nchini Bw David Maraga, alisema Jumatano kwamba serikali inatarajia kujenga mahakama 290 ambapo angalau kila kaunti ndogo itanufaika.
“Tumegundua ya kwamba kesi nyingi zimekwama mahakamani kwa muda mrefu na ni vyema kupunguza mzigo huo,” alisema Bw Maraga.
Aliyasema hayo kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa mahakama mpya ya kaunti ndogo ya Ruiru, iliyoorodheshwa rasmi katika gazeti la serikali mnamo Aprili Mosi 2019.
Alimpongeza kinara wa mahakama hiyo ya Ruiru Bi Clara Omondi kwa kuisimamia kwa ustadi mkubwa.
Jaji Maraga alisema kwa muda wa miezi minne tangu mahakama hiyo kuanza kazi rasmi, kati ya kesi 3,400 zilizowasilishwa katika mahakama hiyo tayari 2,700 zimesikilizwa, zikaamuliwa na kukamilika.
Alizihimiza idara zote za serikali zishirikiane ili kurahishisha kazi muhimu ambayo ni kuwahudumia wananchi.
“Sitaki kuona kesi ambazo zinarundikana mahakamani na kuchukua muda mrefu kabla ya kukamilika kwazo. Majaji na mawakili wanastahili kuona ya kwamba hakuna tabia ya kuahirisha kesi kila mara kwani kufanya hivyo kunamnyima haki mlalamishi na hata mshtakiwa ,” alisema Bw Maraga.
Alishauri mahakama na familia zinazofuatilia kesi za urithi kuhakikisha kesi zinakamilika haraka iwezekanavyo bila kuchukua miaka na mikaka kortini.
Hekina na juhudi
Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara alimpongeza Jaji Maraga kwa hekima yake ya kufanya juhudi na kufungua rasmi mahakama mpya ya Ruiru.
“Ruiru itafaidika pakubwa kwa kupata heshima kubwa ya kupewa mahakama yake. Kwa hivyo ninaomba ushirikiano wa kila mmoja ili tusonge mbele,” alisema Bw King’ara.
Alisema mji wa Ruiru – na sungosungo zake – una idadi ya wakazi wapatao 617,000 huku ikijumuisha makabila na tabaka mbalimbali.
Alifafanua kuwa jambo muhimu linaloupa mji wa Ruiru uhai ni barabara kuu ya Thika Superhighway ambayo hutumiwa na wasafiri zaidi ya milioni moja kila siku.
Alisema mji wa Ruiru una viwanda vipatavyo 53 na vimeajiri wafanyakazi zaidi ya 83,000.
Alieleza kuwa hapo awali mji huo ulikuwa maarufu katika uzalishaji wa mazao kama kahawa, kilimo cha makonge na miwa lakini siku hizi ni eneo kubwa la biashara na ununuzi wa vipande vya ardhi.
Jaji mkuu Kiambu, Bi Christine Meoli alipongeza kazi nzuri inayoendeshwa na mahakama mpya ya Ruiru.
Alisema tangu mwezi Aprili 2019 mahakama ya Ruiru imesaidia katika kukusanya ushuru wa takribani Sh8 milioni.
“Tuna matumaini kuwa mahakama hii itatatua kesi za washuikiwa kwa haraka ili haki ipatikane kwa kila mmoja,” alisema jaji huyo.