• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:50 AM
Huenda Raila akasema ‘Matiang’i tosha 2022’

Huenda Raila akasema ‘Matiang’i tosha 2022’

Na RUTH MBULA na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Waziri Mkuu Raila Odinga amedokeza Ijumaa kuwa huenda akamwidhinisha Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kwa wadhifa wa urais wakati ukifikia.

Huku akimtaja waziri huyo kama mwana wake ambaye alimjua tangu zamani, Bw Odinga alisema kumtawaza wakati huu kutaharibu malengo ya muafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta, almaarufu, handisheki.

“Huyu ni kijana mchapakazi. Kwa hivyo, msinikumbushe kile ambacho ninapaswa kufanya. Lakini wakati mwafaka haujatimia. Tulieni,” Bw Odinga akawaambia waombolezaji kwenye mazishi ya aliyekuwa waziri msaidizi Hezron Manduku.

Mazishi hayo yalifanyika nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Nyaturago, eneobunge la Nyaribari Masaba, Kaunti ya Kisii.

Hatua ya Rais Kenyatta kupandisha cheo kwa Dkt Matiang’i kuwa Mkuu wa Mawaziri kumemfanya kuwa kivutio kwa wanasiasa, hasa kutoka eneo la Gusii anakotoka, ambao sasa wanamsukuma kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Lakini Dkt Matiang’i, kama zamani, hajasema lolote kuhusu suala hilo japo tayari amekubali kutawazwa na wazee wa jamii ya Ekegusi kuwa msemaji wa jamii katika masuala ya uongozi na maendeleo.

Na Ijumaa, Waziri huyo ambaye alikuwa na Bw Odinga, pamoja na viongozi wengine kutoka eneo hilo katika mazishi hayo, alitoa wito kwa viongozoi kulenga masuala ya maendeleo pekee.

“Tuwe na mwelekeo, sharti tuhakikishe kuwa mambo yanaenda shwari. Tulenge masuala ya maendeleo jinsi Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wameshauri,” akasema.

Kuidhinisha

Lakini viongozi waliohutubu wakiongozwa na Gavana James Ongwae (Kisii) na mwenzake wa Nyamira John Nyagarama walimtaka Bw Odinga kumwidhinisha “mwana wetu” kwa wadhifa wa urais 2022.

Walimtaka kiongozi huyo wa ODM kufanya kazi kwa karibu na Dkt Matiang’i ili kumfundisha mbinu faafu za uongozi.

Bw Ongwae alisema Waziri huyo ameonyesha mfano mzuri wa uongozi katika utumishi wa umma na kupandishwa kwake cheo kutawafaa watu wa jamii ya Gusii.

“Tuko na mwana wetu ambaye amehitimu kuwa Rais. Mkenya kutoka Kisii sasa ameiva na anaweza kuingia Ikulu 2022. Tunakuomba umuunge mkono,” Gavana Nyagarama akamwambia Bw Odinga.

Mbunge wa Borabu Ben Momanyi alibashiri kuwa “Ikulu” ijayo itakuwa katika eneobunge lake. Dkt Matiang’i anatoka eneobunge la Borabu.

Mbunge huyo aliwakumbusha waombolezaji kwamba Dkt Matiang’i alipandishwa cheo kwa sababu ni mchapakazi akilinganishwa na mawaziri wenzake, sifa ambayo inafaa kutambuliwa kwa kupigwa jeki ili aingie Ikulu.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Gavana wa Migori Okoth Obado, naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi, Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro na madiwani kadhaa kutoka kaunti za Kisii na Nyamira.

You can share this post!

Chepkoech ahifadhi taji la Diamond League, avuna Sh5.1...

Mawakili 35 waenda kortini kupinga kufurushwa kwa familia...

adminleo