JAMVI: Njama za Raila na Moi kuzima Ruto
Na WANDERI KAMAU
MPANGO wa serikali kuanza kuwahamisha tena wenyeji wa Bonde la Ufa kutoka msitu tata wa Mau, unaonekana kama harakati mpya za kumchapa kiboko cha kisiasa Naibu Rais William Ruto.
Wakazi wengi wanaokaa na kuendesha kilimo katika msitu huo ni wa kutoka jamii ya Wakipsigis na Maasai, ambazo ni mojawapo wa zile ambazo zimekuwa zikimuunga mkono kisiasa Dkt Ruto.
Mpango huo ulitangazwa mapema wiki hii na Mshirikishi Mkuu wa shughuli za serikali katika ukanda huo Bw George Natembeya, akionekana kuwajibu washirika kadhaa wa karibu wa Dkt Ruto, ambao Jumapili iliyopita waliukosoa vikali.
Viongozi hao ni Seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), magavana Paul Chepkwony (Kericho), Hillary Barchok (Bomet) na wabunge kadhaa.
Bw Murkomen alisema kwamba ikiwa serikali ya Jubilee itauendesha mpango huo, basi itakuwa sawa na kuwasaliti wenyeji hao, ikizingatiwa kuwa Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto waliwaahidi wakati wa kampeni zao mnamo 2017 kwamba hawatawahamisha.
“Tunaomba serikali kuheshimu haki za wakazi kumiliki mashamba na kuendesha kilimo. Hatutaki wakazi wetu kudhulumiwa kwa kisingizio cha kuhifadhi msitu huu,” akasema Bw Murkomen.
Licha ya malalamishi yao, Jamvi la Siasa limebaini kwamba mpango huo unaendeshwa kichinichini ili kuzua taswira kwamba Dkt Ruto ameshindwa kuwatetea wakazi hao, ambao walimuunga mkono kwenye chaguzi kuu za 2007, 2013 na 2017.
Duru vilevile zinaeleza kwamba kuna mkono fiche wa kiongozi wa ODM Raila Odinga na Seneta Gideon Moi wa Baringo kwenye mpango huo, wakilenga kumzima kisiasa Dkt Ruto miongoni mwa jamii ya Wakalenjin.
Kiongozi wa Chama Cha Mashinani (CCM) Isaac Ruto tayari amefichua kwamba baadhi ya viongozi wa eneo hilo wamekutana na Mabwana Odinga na Moi, kwenye msururu wa mikutano inayoaminika kujadili mikakati ya kusuluhisha mzozo huo.
Wanasiasa waliokuwepo kwenye ujumbe huo ni mawaziri wa zamani Zakayo Cheruiyot, Franklin Bett, Musa Sirma, Magerer Langat, Paul Sang na wazee kadhaa kutoka jamii ya Wakelenjin.
Bw Ruto, ambaye alihudumu kama gavana wa Bomet alisema kwamba kufuatia mkutano huo, wataandaa mikutano mingine mingi kwa kuwashirikisha viongozi wa eneo hilo na wa kitaifa.
“Tutawashirikisha viongozi zaidi ili kuhakikisha kuwa hakuna mkazi ambaye atadhulumiwa kwa namna yoyote kwenye shuhghuli hiyo,” akasema Bw Ruto
Hata hivyo, kutengwa kwa Dkt Ruto kwenye mchakato huo kumeibua maswali kuwa unatumiwa kumpiga kiboko kisiasa, kwa kumsawiri kama aliyeshindwa kutetea maslahi ya jamii ya Wakipsigis.
Kulingana na Bw Kiprotich Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za Bonde la Ufa, uhamisho huo ni sehemu ya mikakati mingi ya kisiasa ambayo inatumiwa kumyumbisha Ruto, hasa katika eneo hilo ambalo ni ngome yake ya kisiasa ielekeapo 2022.
“Dkt Ruto hajatajwa kwa vyovyote vile kwenye mpango huo. Kilicho wazi ni kuwa msitu huu unatumiwa kumpiga kisiasa, ikizingatiwa kuwa Wakipsigis wamekuwa wafuasi wake tangu mwaka 2007,” asema Bw Mutai.
Wakipsigis wengi walio katika msitu huo walitoka katika kaunti za Bomet na Kericho, ambapo walipewa makao na serikali katika msitu huo kwa lengo la kusimamia na kuendelesha uhifadhi wake.
Wachanganuzi wanasema kuwa ziara za mara kwa mara ambazo Bw Odinga amekuwa akifanya katika ukanda huo ni ishara kwamba lengo lake kuu ni kumkata miguu kisiasa kabisa Dkt Ruto.
Vilevile, wanasema kuwa Bw Odinga analenga kuutumia kulipiza kisasi dhidi ya Dkt Ruto, ikizingatiwa kuwa hatua yake kuunga mkono kuhamishwa kwa wenyeji mnamo 2012 ndiko kulichangia kushindwa kwake kwenye uchaguzi wa 2013.
“Msimamo wa Raila akiwa Waziri Mkuu kwenye serikali ya mseto kati yake na Rais Mstaafu Mwai Kibaki ndiko kulichangia yeye kupoteza umaarufu miongoni mwa Wakalenjin, hali iliyosababisha kushindwa kwake kwenye uchaguzi wa urais wa 2013. Vivyo hivyo, mkakati wake ni kulipiza kisasi dhidi ya Dkt Ruto,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.
Wachanganuzi pia wanasema kuhusika kwa Seneta Moi kwenye mchakato huo vilevile ni kulipiza kisasi dhidi ya Dkt Ruto, ikizingatiwa alichangia sana kushindwa kwa wanawe Rais Mstaafu Daniel Moi mnamo 2007 kutokana na wimbi kubwa la chama cha ODM katika ukanda wa Bonde la Ufa.
Mnamo 2007, wanawe Moi; Gideon, Raymond Moi na Jonathan Toroitich walishindwa kupata ubunge katika maeneo mbalimbali waliyowania kutokana na wimbi kubwa la ODM, wakati huo Dkt Ruto akiwa kiongozi wake mkuu.
Gideon alishindwa na Sammy Mwaita (ODM) katika eneobunge la Baringo ya Kati, Bw Raymond Moi akashindwa na Luka Kigen (ODM) katika eneobunge la Rongai, huku Jonathan Toroitich akishindwa na Moses Lessonet (ODM) katika eneo la Eldama Ravine.
“Hivyo, kuungana kwa Bw Odinga na Seneta Moi dhidi ya Dkt Ruto kwenye suala la Mau ni mkakati wa kulipiza kisasi, ikizingatiwa wote wawili ‘wameumia’ mikononi mwake,” asema Bw Muga.
Hata hivyo, baadhi ya washirika wa Dkt Ruto wanashikilia kwamba kitakuwa kibarua kwa viongozi hao kutikisa uungwaji mkono wake katika Bonde la Ufa.