• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:10 PM
Hakuna mzaha, maafisa wa KFS waanza kuingia Mau

Hakuna mzaha, maafisa wa KFS waanza kuingia Mau

Na GEORGE SAYAGIE

DALILI kwamba serikali haina mzaha na mpango wa kuzihamisha familia zinazoishi ndani ya msitu wa Mau, zilidhihirika Jumapili baada ya maafisa wa Shirika la Msitu Nchini (KFS) kuwasili wakiwa ndani ya malori kwa maandalizi ya shughuli hiyo.

Hayo yanajiri huku serikali ikiwapa makataa ya hadi Oktoba 31 familia zinazoishi ndani ya Mau kufunganya virango na kuondoka la sivyo ziondolewe kwa nguvu.

Kuwasili kwa maafisa wa KFS sasa kunaonyesha tangazo la awali la Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko kuwa juhudi za kuuokoa msitu huo lazima zitekelezwe na serikali liwe liwalo.

Hapo jana, zaidi ya maafisa 100 wa KFS waliiingia ndani ya msitu huo na kukita kambi katika maeneo matatu ili kuzirai zaidi ya familia 10,000 ziondoke msituni humo kabla ya makataa hayo ya siku 60.

Taifa Leo ilikumbana na msafara wa maafisa hao katika mzunguko wa TM, kilomita nne kutoka mji wa Narok. Maafisa hao walipitia mzunguko wa Oloulunga na kuelekea msitu wa Maasai Mau.

Ingawa alisema haruhusiwi kuzungumza suala hilo na wanahabari, aliyekuwa Naibu Afisa anayehusika na Uhifadhi wa Misitu Nchini Alex Lemarkoko alionekana kiongozi wa msafara huo kwa kuwa alikuwa akiwaelekeza wakiingia Mau.

Zaidi ya familia 60 kutoka jamii ya Maasai walibeba mali yao na kuanza kuondoka, muda wa saa mbili pekee baada ya maafisa wa KFS kuingia msituni.

Hali hiyo iliibua taharuki katika vijiji kadhaa ijapokuwa kutekelezwa kwa uhamisho kikamilifu bado haukuwa umeanza.

Bw Moses Ole Kiok ambaye alikuwa na ekari 80 katika ranchi ya Enkaroni ndani ya Mau alisema aliamua kutii agizo la serikali kwa hiari na kutoa wito kwa wakazi wengine pia kujiondoa kabla ya Oktoba 31.

Kuwasili kwa maafisa hao ni ishara kwamba serikali itawahamisha wanaoishi msituni, wiki mbili baada ya kutangaza kwenye magazeti kwamba hatimiliki 1,274 za watu wanaoishi Mau ni feki.

Haya yanajiri huku viongozi kutoka jamii ya Kalenjin wakipinga kutekelezwa kwa oparesheni hiyo.

You can share this post!

Lazima Ruto aingie Ikulu – Tangatanga

Wahariri waonya wanaodhuru wanahabari

adminleo