TAHARIRI: Mzozo wa seneti na bunge unaumiza raia
NA MHARIRI
Magavana wamesema kwa yakini kwamba shughuli katika kaunti zote 47 zitavurugika kuanzia Septemba 16 iwapo mabunge ya Seneti na Kitaifa hayatakuwa yamesuluhisha utata unaozingira Mswada wa Ugavi wa Mapato wa 2019.
Ukweli ni kwamba huduma muhimu kwa wananchi na taifa kwa jumla zitasambaratika kama kweli hapatakuwa na mwafaka kuhusu suala hili nyeti.
Migongano hii imesababisha Sh50 bilioni kusalia katika Hazina ya Kitaifa huku wabunge na maseneta wakizozana kuhusu kiwango cha fedha wanachotaka kuidhinisha. Wakenya wanaotegemea serikali za kaunti kupata huduma zao wanaendelea kupata shida makabiliano haya yanapoendelea kushamiri.
Isitoshe, kando na mitafaruku ya seneti na bunge la kitaifa, hali imeendelea kuwa mbaya zaidi kutokana na uamuzi wa Hazina ya Kitaifa na Baraza la Magavana kughairi kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Ugavi wa Mapato.
Baya zaidi ni kwamba wabunge wako likizoni hivyo hawawezi kujadili masuala hayo muhimu na hivyo kurefusha mjadala unaoyazunguka na pia kupata suluhu ya shida hii.
Uchechefu huu wa pesa unatishia kuua ugatuzi kwa sababu bila ya fedha utendakazi wa kaunti utalemazwa, miradi itasitishwa, mishahara itakosekana na hilo litawaingiza vijana kwenye uhalifu wa hali ya juu ili kujikimu kimaisha. Uhalifu nao utakuwa unahatarisha maisha yao na ya wawategemeao.
Vifo vitaongezeka kutokana na ukosefu wa huduma za kiafya na dawa kwa wakazi.
Shughuli za kibiashara katika kaunti mbalimbali nchini zaelekea kukwama wa sababu kaunti sasa haziwezi kuwalipa wasambazaji na wakandarasi mbalimbali. Zigo la madeni linazidi kuzonga kaunti kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu ugatuzi uanze.
Pesa zinazoibua mzozo huu mkubwa si nyiingi vile. Linalodhihirika hapa wazi ni ubinafsi wa viongozi wasiojali maslahi ya raia wa kawaida, wananchi walioamka mapema Agosti 2017 kuwapigia kura. Ni wakati bora wadau wote waketi pamoja kikaoni kutafuta suluhu la kudumu kwa zahama hii.
Wabunge na maseneta waache misimamo yao mikali, nao magavana waondoe kesi kortini, wakubali Sh316 bilioni ambazo Hazina Kuu inasema ndizo zipo, na kazi iendelee