Mifuko ya plastiki inavoingizwa nchini kisiri
Na GERALD BWISA
MIFUKO ya plastiki iliyopigwa marufuku nchini bado inatumiwa kwa wingi katika Kaunti ya Trans Nzoia huku wakazi wakiinunua kutoka nchi jirani ya Uganda.
Wafanyabiashara walaghai wanaingiza nchini mifuko hiyo kupitia mpaka wa Suam.
Waziri wa Mazingira wa Trans-Nzoia Maurice Lokwaliwa alisema uchunguzi wa serikali ya kaunti ulibaini mifuko hiyo inafichwa ndani ya bidhaa nyinginezo zinazoingizwa nchini kutoka Uganda.
“Tutashirikiana na Mamalaka ya Mazingira (Nema) kuhakikisha wafanyabiashara wanaouza mifuko hiyo iliyopigwa marufuku wanakamatwa,” akasema Bw Lokwaliwa wakati wa kuadhimisha siku ya mazingira katika shule ya msingi ya Kitale Union.
Aliitaka mamlaka ya Nema kupiga marufuku matumizi ya aina zote za plastiki ikiwemo mirija inayotumika kunywa soda au maziwa.