• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Dalili kaunti inavunja urafiki na Ruto

Dalili kaunti inavunja urafiki na Ruto

Na EVANS KIPKURA

WAKAZI wa Elgeyo-Marakwet wameanza kuachana na Naibu Rais William Ruto na kukaribisha kufunguliwa upya kwa afisi ya chama cha ODM mjini Iten.

Katika hatua inayoonekana kutokuwa ya kawaida, Kinara wa ODM Raila Odinga amezuru eneo hilo mara mbili tangu Julai, na sasa anatarajiwa kufungua rasmi ofisi hiyo mwishoni mwa mwezi huu.

Wafuasi wa chama cha Jubilee wamedidimia eneo hilo, kutokana na kashfa za ufisadi zinazoandama miradi ya mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Katika siku za hivi majuzi, Gavana Alex Tolgos ameonekana kumtema Dkt Ruto, ambaye alishabikiwa sana eneo hilo haswa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, na kumuunga mkono Bw Ondiga.

Kabla ya uchaguzi wa 2007, chama cha ODM kilionekana kuwa maarufu eneo la Elgeyo-Marakwet lakini baada ya uhusiano wa Bw Ruto na Odinga kuvunjika, wafuasi wengi walionekana wakiegemea upande wa chama cha Jubilee.

Ofisi mpya ya ODM imeonekana kufanyiwa marekebisho na kuboreshwa hata zaidi kwa maandalizi ya kuwasajili wanachama zaidi kutoka eneo hilo.

Mwenyekiti wa chama hicho eneo hilo Bw Micah Kigen alisema mipango na maandalizi yako katika awamu za mwisho mwisho na hivi karibuni ofisi hiyo itapakwa rangi rasmi za chama cha Chungwa.

“Tunatumai tutaanza kazi hapa kabla ya mwisho wa mwezi huu. Tutaajiri afisa msaidizi kwenye ofisi hii ili atusaidie kuhakikisha kuwa mambo yanasonga vyema na wageni wowote wanashughulikiwa ipasavyo,” akasema Bw Kigen.

You can share this post!

Shinikizo viongozi wafisaadi SDA wakamatwe

Kutuny, Kamanda na Moses Kuria wapinga uteuzi wa Mariga

adminleo