• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Lusaka awataka viongozi waeleze faida ya miswada

Lusaka awataka viongozi waeleze faida ya miswada

DENNIS LUBANGA na GERALD BWISA

SPIKA wa Bunge la Seneti, Bw Ken Lusaka amewaomba viongozi wa kisiasa nchini kuwahamasisha Wakenya kuhusu manufaa ya ripoti inayosubiriwa ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) na mswada wa Punguza Mizigo unaovumishwa na Kinara wa Thirdway Alliance, Dkt Ekuru Aukot.

Bw Lusaka ambaye alijitaja kama ‘refa’ kwenye mjadala unaoendelea kuhusu BBI na Punguza Mizigo, alisema Wakenya wengi hawafahamu kilichomo kwenye miswada hiyo miwili huku viongozi nao wakianza harakati ya kuwarai kuipinga au kuinga mkono wakati wa kura ya maamuzi.

“Kwa kuwa mimi ndiye nitakuwa refa kuhusu miswada ya Punguza Mizigo na BBI, ombi langu kwa viongozi ni kuwa wanafaa kuandaa hamasisho kuhusu miswada hii na kuwaeleza Wakenya manufaa watakayopata kwa sababu hilo ndilo muhimu zaidi kwenye mjadala huu,” akasema.

Aidha, alisisitiza kwamba Wakenya bado hawajui lolote kuhusu BBI na Punguza Mizigo na wanafaa kuelezwa namna miswada hiyo itakavyowapunguzia gharama ya maisha.

Bw Lusaka alikuwa akiwahutubia waombolezaji katika kijiji cha Sikhendu, Kaunti ya Trans Nzoia wakati wa mazishi ya mama Jennifer Washiali aliye dada yake Kiranja wa Wengi kwenye Bunge la Kitaifa, Ben Washiali.

Bw Lusaka, ambaye alikuwa gavana wa Bungoma kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, pia aliahidi kufanya kazi na viongozi kutoka mirengo yote ya kisiasa kuhakikisha kuwa maslahi ya raia yanatimizwa nchini.

“Kama viongozi tunafaa kutumia nafasi ambazo Mungu ametupa kuwasaidia watu wetu. Hii ni kwa sababu sisi sote tuna rasilimali na uwezo wa kuinua hali ya maisha ya watu wetu,” akaongeza.

Akizungumza kwenye mazishi hayo, Mbunge wa Kimilili, BW Didmus Barasa alitangaza hadharani kuwa atapinga ripoti ya BBI iwapo haitaangazia jinsi ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili Wakenya.

“Nitasoma kwa kina ripoti ya BBI ili nifahamu iwapo imependekeza njia za kubadilisha maisha ya Wakenya au la. Nitaipinga iwapo haitatimiza vigezo hivyo kwa sababu tunataka pesa zaidi zitengewe kaunti ili kusaidia mwananchi wa kawaida,” akasema Bw Barasa.

Mbunge huyo ambaye pia ni mwandani wa kisiasa wa Naibu Rais Dkt William Ruto alisema matatizo yanayowakabili Wakenya hayatokani na kasoro kwenye sheria bali ulafi wa viongozi wa kisiasa nchini.

“Tunataka viongozi ambao hawana tamaa ya mali na watakaongozwa na wito wa kuwasaidia Wakenya na kuimarisha hali yao ya maisha,” akaongeza Bw Barasa.

Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa hata hivyo alisema Bunge la Kitaifa litatupilia mbali mswada wa Punguza Mizigo kwa sababu unapendekeza kufutiliwa mbali kwa maeneobunge, hali ambayo itawakosesha wabunge kazi ya kutunga sheria.

“Tumeyaona mapendekezo ya Punguza Mizigo na hapa Trans Nzoia tuna maeneobunge matano ambayo mswada huu unapendekeza yavunjwe. Tunamwambia Dkt Aukot kwamba duniani uwakilishi wa raia huongezwa ndiyo maana tunasema mswada huo hautafika popote,” akasema Bw Wamalwa.

You can share this post!

Kutuny, Kamanda na Moses Kuria wapinga uteuzi wa Mariga

Waajiri wahimizwa wafidie waandishi wanapovamiwa

adminleo