Mauaji ya wageni Afrika Kusini yazua ghadhabu barani
Na MASHIRIKA
MAUAJI yanayolenga raia wa kigeni nchini Afrika Kusini yamezua ghadhabu katika mataifa mbalimbali ya Afrika huku idadi ya waliouawa kinyama ikifikia watu saba.
Umoja wa Afrika (AU) ulishutumu vurugu dhidi ya raia wa kigeni zinazoendelea jijini Johannesburg, huku ukisema kuwa wafanyabiashara ambao wamepata hasara katika machafuko hayo wanafaa kulipwa fidia.
Watu wasiopungua 80 wamekamatwa kufuatia vurugu hizo ambapo mamia ya vijana walivamia na kupora biashara zinazomilikiwa na raia wa kigeni.
Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa AU Moussa Faki Mahamat, alipongeza serikali ya Afrika Kusini kwa kuwakamata wahusika wa vurugu hizo.
“Serikali ya Afrika Kusini haina budi kulinda maisha na mali ya Waafrika wenzao. Umoja wa Afrika uko tayari kusaidia,” akasema Bw Faki.
Rais wa Zambia Edgar Lungu aliitaka serikali ya Afrika Kusini kukomesha vurugu hizo mara moja.
“Nawasihi raia wa Zambia humu nchini na ughaibuni kutowadhuru raia wa Afrika Kusini walio karibu nao. Tulaani unyama unaotendeka nchini humo bila kuzua fujo,” akasema Rais Lungu kupitia mtandao wa Facebook.
Rais Lungu alitoa kauli hiyo baada ya raia wa Zambia kuandamana jijini Lusaka na kupora maduka yanayomilikiwa na raia wa Afrika Kusini.
Shirikisho la Kandanda nchini Zambia (Faz) lilifutilia mbali mechi ya kirafiki baina ya timu ya nchi hiyo (Chipolopolo na ile ya Afrika Kusini (Bafana Bafana) iliyofaa kuchezwa Jumamosi jijini Lusaka.
Shirikisho hilo lilifutilia mbali mechi hiyo baada ya raia kulishinikiza kuitupilia mbali kama njia mojawapo ya kupinga mauaji ya kinyama na uharibifu wa mali jijini Johannesburg.
Wakati huo huo, polisi nchini Nigeria jana walidumisha usalama katika biashara zinazomilikiwa na raia wa Afrika Kusini jijini Abuja kutokana na hofu kwamba huenda zikavamiwa.
Polisi walishika doria nje ya maduka na afisi za mtandao wa simu wa MTN unaomilikiwa na Afrika Kusini.
Mtandao wa MTN, hata hivyo, ulikuwa umefunga afisi zake zote jijini Abuja kwa kuhofia kushambuliwa.
“Tumefunga kwa kuhofia usalama wa wafanyakazi na wateja wetu,” ikasema notisi iliyobandikwa nje ya afisi hizo.
Jumanne, watu waliokuwa na ghadhabu walivamia na kupora mali katika duka linalomilikiwa na raia wa Afrika Kusini jijini Lagos, Nigeria.
Wasanii kadhaa, akiwemo mwanamuziki Tiwa Savage wa Nigeria wamefutilia mbali matamasha waliyofaa kutumbuiza nchini Afrika Kusini.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Jumanne alilaani vurugu hizo huku akisema kuwa zinatia doa sifa ya Afrika Kusini.