• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
WANGARI: Mahakama zitumie teknolojia kuimarisha huduma zao

WANGARI: Mahakama zitumie teknolojia kuimarisha huduma zao

NA MARY WANGARI

Hivi majuzi, Jaji Mkuu David Maraga alifichua kwamba mahakama zimefanikiwa kupunguza mrundiko wa kesi zilizodumu kwa miaka mitano kutoka 110,000 hadi kesi 15,278 pekee.

Bila shaka hizi ni habari za kutia moyo, hasa wakati huu ambapo juhudi za kuifanyia mageuzi idara ya mahakama zinapoendelea.

Hata hivyo, uhalisia uliopo ni kwamba, kwa muda mrefu, mchakato wa kupata haki nchini umekuwa mrefu, wa kuchosha na aghalabu unaowaacha wengi wametamauka.

Sawa na msemo maarufu ‘haki kuchelewa ni kunyimwa haki” hakuna kinachoumiza zaidi kama kufuatilia kesi mwaka baada ya mwaka kwa lengo la kupata haki bila mafanikio.

Hali hii humwacha mlalamishi akiwa amethirika kisaikolojia na hata kifedha kwa kuwa masuala ya kutafuta haki ni ghali mno nchini. Cha kuudhi zaidi ni wakati mlalamishi anapoelezwa kwamba faili ya kesi husika imetoweka ghafla baada ya mshtakiwa na baadhi ya maafisa fisadi kortini kushirikiana kuhujumu utekelezaji wa haki.

Kutokana na hali hii pana haja kubwa ya kushirikisha teknolojia katika utoaji huduma za mahakama nchini. Kuanzisha mfumo wa kidijitali katika uendeshaji wa shughuli za mahakama utasaidia pakubwa katika kuharakisha utoaji wa haki kwa wahasiriwa.

Inashangaza kwamba, katika karne hii ya 21 ya utandawazi na maendeleo kiteknolojia, tungali tumesalia nyuma katika mbinu za kale za kuhifadhi ushahidi na rekodi muhimu za mahakama kwenye faili.

Huku tukifahamu kwamba idara ya mahakama ni mojawapo wa matawi makuu katika uongozi wa taifa, hatuna budi kuandamana na majira la sivyo tutaendelea kusalia nyuma.

Idara ya mahakama imegubikwa na visa vya kushangaza vinavyomwacha raia wa kawaida ametamauka asijue wapi pengine pa kukimbilia ili kupata haki. Kumekuwepo visa chungu nzima kuhusu faili za kesi kutoweka. Aidha, visa vya stakabadhi muhimu kama vile hati za kumiliki ardhi kutoweka ghafla kutoka kwenye sajili ya korti na kisha nakala hizo kutumika kama dhamana ya kuwaachilia huru wahalifu sugu ni jambo la kawaida.

Mfumo wa haki katika taifa unapaswa kuhakikisha usawa kwa wote ambapo haki inatendeka bila kuegemea upande wowote iwe ni tajiri au fukara. Nyakati ambapo watu wachache katika jamii walitendewa haki zimepitwa na wakati.

Hatuwezi kupuuza ukweli kwamba, idara ya mahakama bila shaka imepiga hatua kubwa ambapo watu maarufu na viongozi mashuhuri wanashtakiwa, na hata kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia.

[email protected]

You can share this post!

Mauaji ya wageni Afrika Kusini yazua ghadhabu barani

Mau: Murkomen awakaripia Tobiko na Natembeya

adminleo