Hekima ya seneti yafungulia magavana mifereji ya fedha
Na CHARLES WASONGA
MAGAVANA nchini sasa wanaweza kupumua baada ya maseneta kulegeza msimamo wao na kukubali mgao wa Sh316.5 bilioni kwa kaunti jinsi ilivyopendekezwa na wabunge na serikali kuu.
Hatua hiyo ya busara iliyochukuliwa Alhamisi sasa imemaliza mvutano kuhusu suala hilo na kaunti zinatarajia kuanza kupokea fedha hizo kuanzia wiki ijayo bunge la kitaifa litakaporejelea vikao vyake.
Mswada mpya wa ugavi wa fedha (DoRB) uliopendekeza kiasi hicho cha fedha sasa utawasilishwa katika seneti ili upitishwe kabla ya kutiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta.?Awali, maseneta walikuwa wamependekeza kaunti zipewe mgao wa Sh335.7 bilioni katika bajeti ya sasa ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020. Kiasi hicho ndicho kilikuwa kimewekwa na Tume ya Ugavi wa Rasilimali (CRA).
Lakini maseneta jana walilegeza msimamo baada ya mkutano wao uliotishwa na Spika wao Ken Lusaka.?Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen alisema wamefanya “uamuzi huo mchungu” ili kuzuia uwezekano wa kusitishwa kwa shughuli muhimu katika kaunti.
“Fedha hizo hazitoshi, lakini ni afadhali na seneti itaendelea kupigania fedha zaidi wakati mwingine. Seneti haitaruhusu ugatuzi ambao ndio nguzo kuu ya Katiba yetu kuhujumiwa kupitia njama fulani,” Bw Murkomen akasema.
Mvutano umekuwa ukiendelea kuhusu suala hilo tangu Juni, hali iliyopelekea bajeti ya mwaka huu kusomwa kabla ya kupitishwa kwa mswada wa ugavi wa fedha.?Awali, bunge la kitaifa lilipendekeza mgao wa Sh310 bilioni kwa kaunti, lakini baadaye likaongeza kiasi hicho hadi 316.5 bilioni baada ya kamati ya maridhiano kuundwa kutafuta muafaka kuhusu suala hilo.
Nao maseneta walipunguza kiasi cha fedha walichopendekeza hadi Sh327.7 bilion, ndipo wakakosa kuelewana na wabunge.
Kutoelewana huko ndiko kulisababisha Waziri wa Fedha aliyesimamishwa kazi Henry Rotich kusoma bajeti, Juni 13, iliyotenga Sh310 bilioni kwa kaunti.? Na mwezi jana, Bunge la Kitaifa, kupitia kamati kuhusu bajeti, lilitayarisha mswada mwingine wa ugavi wa fedha likizitengea serikali Sh316.5 bilioni, kiasi ambacho Rais Kenyatta aliunga mkono.
Kiongozi wa taifa alisema serikali haina fedha za kuongeza serikali za kaunti. Akasema alipohudhuria mazishi ya mamake mwanasiasa Peter Kenneth: “Nyinyi wabunge mwaweza kupunguza mishahara yenu na mzipe kaunti pesa zaidi. Lakini mimi sina pesa za kuwaongezea!”?Mvutano kuhusu suala hilo ulichochea magavana kwenda katika Mahakama ya Juu wakitaka ushauri kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, majaji wa mahakama hiyo, wakiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga, walisema suala hili linaweza tu kutatuliwa na mabunge yote mawili sio mahakamani. ?Bw Maraga aliwashauri maspika Justin Muturi na Lusaka kuunda kamati nyingine ya maridhiano kutanzua mvutano huo.
Hata hivyo, kikao cha kwanza cha kamati hiyo, kilichofanyika katika ukumbi wa County, Nairobi, wiki jana kiligeuka uwanja wa vita vya maneno kati ya maseneta na wabunge.
Wawikilishi wa mabunge hayo mawili walishikilia misimamo yao ya awali na hivyo kukosa kuelewana.?Hii ndio maana wiki jana mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya alitangaza kuwa serikali zote za kaunti zitasitisha shughuli ifikapo tarehe 16 mwezi huo ikiwa muafaka hautapatikana kuhusu suala hilo.