Wizara ya Afya yaanza kutoa chanjo ya Hepatitis B kwa wakazi
DENIS LUBANGA na JOAN MURUGI
WAHUDUMU kutoka Wizara ya Afya wameanza kampeni ya kuwapa chanjo wakazi wa eneo la Mlima Elgon, Kaunti ya Bungoma dhidi ya ugonjwa wa Hepatitis B.
Hii ni baada ya ripoti kadhaa za mkurupuko wa ugonjwa huo katika eneo hilo.
Tayari, watu 22 wamebainika kuambukizwa virusi vya maradhi hayo. Kando na hayo, wakazi wanaendelea kuomboleza kifo cha Bi Edna Chebisis, 40, aliyefariki pia kutokana na ugonjwa huo wiki tatu zilizopita.
Maafisa wanaosimamia shughuli hizo wamewahakikishia wakazi kwamba wanafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa wamedhibiti hali hiyo kabla iwe mbaya zaidi.
Ugonjwa huo huathiri ini, na unaweza hata kumfanya mgonjwa kupata saratani. Kulingana na wataalamu, madhara yake yanaweza kuwa mabaya ikiwa mtu anakosa kupata matibabu kwa haraka.
Maradhi hayo husambazwa kupoitia kwa damu ama majimaji kutoka sehemu zingine za mwili za mtu aliyeathirika.
Msimamizi Mkuu wa Huduma za Afya katika Kaunti ya Bungoma, Bw Moses Wangusi alisema jana kuwa wanashirikiana na wenzao kutoka Bunge la Kitaifa kukabili hali hiyo.
“Kwenye sampuli ambazo tuliwasilisha katika Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu Kenya (KEMRI) jijini Nairobi na Hospitali ya Rufaa ya Bungoma, nyingi zilionyesha dalili za ugonjwa huo,” akasema Bw Wangusi kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Mkuu huyo alisema kwamba wamepokea usaidizi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO). Kikosi cha serikali kinawasaidia kwenye taratibu za kutoa chanjo hizo.