• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Orengo akosoa Rais kuhusu mswada wa fedha

Orengo akosoa Rais kuhusu mswada wa fedha

Na DICKENS WASONGA

KIONGOZI wa wachache katika seneti James Orengo amemkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kuingilia utendakazi wa Bunge badala ya kuruhusu asasi hiyo kufanya kazi yake kwa njia huru.

Akiongea mjini Siaya wakati hafla ya kuchanga fedha za kusaidia zaidi ya makundi 200 ya wanawake kutoka kaunti hiyo, Bw Orengo alisema Rais anapaswa kuruhusu mabunge mawili ya Seneti na Bunge la Kitaifa kutekeleza majukumu yao ya kikatiba bila ya kuyaingilia.

“Bunge ni tawi huru la serikali ambalo linapasa kuruhusiwa kuendesha majukumu yake kwa njia huru bila kuelekezwa na afisi ya Rais,” akasema seneta huyo wa Siaya.

Bw Orengo alisema Seneti ilikubali, japo kwa shingo upande mgao wa Sh316.5 bilioni kwa kaunti ulivyopendekezwa na bunge la kitaifa, ili shughuli zisikwame katika serikali hizo.

“Hata kama hakukubaliana na wazo hilo, tulilikubali ili miradi ya maendeleo katika kaunti isikwame,” akasema.

Bw Orengo alisema pesa ambazo hutengewa serikali za kaunti na Hazina ya Kitaifa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ni za wananchi wala sio za Rais na hivyo hana mamlaka ya kuamua kiasi cha fedha kinachopasa kutengewa serikali za kaunti.

Wakati wa mvutano kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato (DoRB) unaoweka kiwango cha fedha zinazopasa kutengewa serikali za kaunti, Rais Kenyatta aliwaambia wale waliokuwa wakitaka kaunti zitengewe pesa zaidi kwamba hakuna fedha za kutimiza matakwa yao.

Bw Orengo hakufurahishwa na msimamo uliochukuliwa na Rais katika mvutano huo wa ugavi wa mapato katika Seneti na Bunge la Kitaifa, ambao nusra uvuruge shughuli katika serikali za kaunti.

Mvutano kati ya mabunge hayo mawili ulitatuliwa Alhamisi baada ya Seneti kubadili msimamo wao wa awali na kukubali kupitisha mswada wa bunge la kitaifa uliopendekeza mgao wa Sh316.5 bilioni kwa kaunti.

Ni kiwango hicho ambacho rais Kenyatta amekuwa akiwataka maseneta na magavana wakubali, akisema “serikali haina pesa za kuwaongezea”.

Lakini Alhamisi Bw Orengo akafoka: Rais hafai kushurutisha au kuelekeza bunge kuhusiana na ni pesa ngapi zinapasa kupelekwa kwa kaunti,” akasema.

You can share this post!

Balozi wa Amerika aonya kuhusu ufisadi

Kinoti atikisa korti tena, atia pingu hakimu

adminleo