• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KIBRA: Mwamko mpya ODM

KIBRA: Mwamko mpya ODM

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM Jumamosi usiku kulimtangaza kakake marehemu Ken Okoth, Benard Imran Okoth, kuwa mpeperushaji bendera yake katika uchaguzi mdogo wa Kibra huku kwa nadra chama hicho kikionyesha mfano mzuri kwa kudumisha amani katika shughuli hiyo.

Huu ni mwamko mpya katika chama hicho kwani wapinzani wake walitarajia shughuli hiyo kukumbwa na ghasia kama hali ilivyokuwa katika kura za mchujo zenye ushindani mkali kuelekea chaguzi zilizopita.

Wakati wa mchujo wa ODM kuteua wagombeaji wake katika uchaguzi mkuu wa 2017, ghasia zilisheheni katika baadhi ya maeneo wakilishi kwenye ngome zake kutokana na madai ya haki na uwazi kutozingatiwa na wagombeaji fulani kupendelewa.

Fujo hizo zilishamiri katika ngome za ODM za Nyanza, Nairobi na Pwani, hali iliyopelekea chama hicho kupoteza baadhi ya viti kadha.

Vile vile, katika mchujo wa Kibra chama hicho kinachoongozwa na Mjumbe wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu miundo msingi Raila Odinga, kilibuni jopo maalum la kusikiza malalamishi ya wagombeaji wasioridhishwa na matokeo ya uteuzi huo, hatua ambayo ni ya kipekee.

“Wagombeaji wenye malalamishi yoyote wanakaribishwa kuyawasilisha kwa wananchama wa jopo hilo katika makao makuu ya chama chetu jumba la Orange siku ya Jumapili (jana). Hata hivyo, tungependa kuwaomba wagombeaji wote kuunga mkono mshindi Bw Imran ili tuweze kuhifadhi kiti hiki cha Kibra,” akasema Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.

Hata hivyo, changamoto kadhaa zilikumba shughuli hivyo baada ya baadhi ya wapiga kura kulalamika kuwa majina yao hayakuwa kwenye sajili rasmi ya wapiga kura.

Hali hiyo, kulingana na Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) Judy Pareno, ilishuhudiwa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura kwa sababu chama kiliamua kwamba ni watu wenye kadi cha uanachama pekee waliruhusiwa kushiriki.

“Tulifikia uamuzi huu, pamoja na wagombeaji wote 10, ili kuzuia zoezi hili kuingiliwa na wafuasi wa vyama pinzani kwa manufaa yao,” akasema mwenyekiti huyo ambaye pia ni Seneta Maalum.

“Lakini baadaye wanachama wetu halisi walisaidika pale tulipoamua tumia sajili ya IEBC, katika baadhi ya vituo,’ akaeleza Bi Pareno.

Kulingana matokeo rasmi yaliyotangazwa na Afisa Msimamizi wa mchujo huo Dkt Julius Oremo, Bw Imran aliwabwaga wenzake tisa kwa kuzoa jumla ya kura 4,382. Alifuatwa kwa umbali na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Dagoreti Peter Orero aliyepata kura 1,218.

John Milla alipata 906, mkurugenzi wa masuala ya vijana katika ODM Benson Musungu alipata kura 524, Christon Odhiamo (417), Tony Ogola (381), Stephen Okello (228), Brian Owino (127), Reuben Ojijo (52) na Erick Obayi (45).

Bw Imran sasa atapambana na mgombeaji wa Jubilee mwanasoka Mcdonald Mariga, Bw Eliud Owalo wa ANC, Khamisi Bitichi wa Ford Kenya na wagombeaji kadha huru katika uchaguzi huo mdogo utakaofanyika Novemba 7.

Hadi tulipokuwa tukienda mitamboni wagombeaji wa ODM walioshindwa katika mchujo huo wa Jumamosi hawakuwa wamewasilisha malalamishi yao kwa jopo hilo la watu watu katika jumba la Orange.

Na Bw Musungu alituma taarifa akikubali kushindwa na kuahidi kumuungano mkono Bw Imran wakati wa kampeni. Vile vile, aliipongeza ODM kwa kuendesha mchujo huo katika mazingira ya amani na “kwa njia huru na haki.”

You can share this post!

Bashir alimiliki ufunguo wa ‘chumba chenye mabilioni’

Maandamano Murang’a baada ya Nyoro kukamatwa

adminleo