• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Sarakasi za Nyoro kanisani zamletea karaha

Sarakasi za Nyoro kanisani zamletea karaha

Na NDUNG GACHANE

VIONGOZI wa makundi ya Kieleweke na Tangatanga Jumapili walikabiliana vikali kwenye hafla ya mchango wa harambee katika kanisa katoliki la Gitui, eneobunge la Kiharu, Kaunti ya Murang’a.

Mbunge wa eneo hilo, Bw Ndindi Nyoro pamoja na wafuasi wake waliwasili kwenye kanisa hilo dakika chache baada ya zaidi ya wabunge 20 wa mrengo wa Kieleweke kufika huku mbunge maalum Maina Kamanda akiwatambulisha viongozi waliokuwepo.

Hata hivyo, vurugu zilianza alipochukua kipaza sauti kutoka kwa Bw Kamanda, akisema kwamba jukumu la kuwatambulisha wageni na wabunge lilikuwa lake kwa sababu yeye ni mbunge wa eneo hilo.

Bw Kamanda alipinga wazo hilo huku Bw Nyoro akikwamilia kipaza sauti na kukataa kuondoka jukwaani kupisha wabunge wengine kuzungumza.

“Siwezi kuwaruhusu watu kutoka Nairobi kuja hapa na kuchukua usukani wa kuendesha mambo katika eneobunge langu kana kwamba wanafahamu eneo hili kuniliko. Mimi ndiye nilichaguliwa na namwambia Bw Kamanda wazi kwamba alete orodha ya wageni ili niweze kuwaita kuhutubu,” akasema Bw Nyoro.

Hapa ndipo Bw Kamanda aliyeonekana kujaa hamaki alisimama na kuelekea kwenye jukwaa na ghafla bin vuu Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Murang’a, Bw Josephat Kinyua pia akaelekea mbele kisha kanisa likageuka uwanja wa fujo.

Juhudi za kasisi John Kibuuru kutuliza ghasia hizo zilizodumu kwa muda wa dakika 10 ziligonga mwamba kwa kuwa kondoo wake waligawanyika kwenye mirengo miwili iliyounga kundi la Bw Kamanda huku jingine likiunga Bw Nyoro.

“Nawaomba kwa jina la mwenyezi Mungu muwe watulivu. Mambo hayajawahi kuharibika kiasi hiki na nawaomba mtulie ili amani idumu,” akasema Kasisi huyo.

Waumini waliounga Bw Kamanda walidai kwamba ni viongozi wanaoegemea mrengo wa Kieleweke ndio walialikwa kwenye mchango huo na si mbunge wao.

“Bw Nyoro hata hakualikwa kwenye mchango huu. Alikuja kuchelewa kisha akaanza kutumia kifua kuendesha hafla isiyo yake. Tunamlaumu kwa hali hii,” akasema Bw George Kamande.

Baada ya hafla hiyo, Bw Nyoro aliwahutubia wanahabari huku polisi wakimsubiri. Punde alipomaliza, walimvamia ili kumkamata lakini wafuasi wake walikuwa wameshamzingira na kumwingiza kwenye gari lake, wakamtorosha.

You can share this post!

Tunatambua umuhimu wa Mau, watu wafurushwe – Chepkut

Wakulima wakataa sheria mpya za kilimo cha kahawa

adminleo