• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Wezi waiba kahawa ya Sh400,000 kiwandani

Wezi waiba kahawa ya Sh400,000 kiwandani

Na GEORGE MUNENE

KAHAWA ya thamani ya Sh400,000 iliibwa jana baada ya wezi kuvamia kiwanda cha Gituto katika Kaunti ya Kirinyaga.

Majambazi hao walivamia kiwanda hicho usiku wa manane na kuwashambuliwa walinzi wawili na kisha kutoweka na kilo 1,000 za kahawa.

Kulingana na Bw Jamleck Kariuki, mmoja wa maafisa kiwandani hapo, wavamizi hao waliwafunga kwa kamba walinzi hao kwenye mti na kuwapiga.

Baadaye walivunja mlango wa stoo na kupakia magunia ya kahawa kwenye lori.

Wizi huo unaosadikiwa kupangwa na baadhi ya maafisa kiwandani hapo umewatia hofu wakulima.

Baada ya wavamizi hao kuondoka, walinzi hao walifanikiwa kujifungua wenyewe na kuripoti kisa hicho kwa usimamizi wa kiwanda hicho.

“Walinzi walikuja leo asubuhi na kutueleza yaliyotokea ndiposa tukaripoti katika kituo cha polisi,” akasema Bw Kariuki.

“Tulisikitika kubaini kwamba kahawa yote iliyokuwa stooni ilichukuliwa na wavamizi hao waliokuwa na silaha. Mmoja wa walinzi alijeruhiwa na wavamizi hao,” akaongezea.

Afisa mwingine katika kiwanda hicho Bw Patrick Muriuki aliwataka maafisa wa polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwanasa waliohusika na mpango wa wizi wa kahawa hiyo.

‘Tunachotaka ni kwamba kahawa hiyo irejeshwe na wahusika wanaswe na kufikishwa mahakamani,” akasema Bw Muriuki.

Polisi wamekamata mameneja wawili wa kiwanda hicho, walinzi wawili na mfanyakazi mmoja wa kibarua kuhusiana na wizi huo.

Wawili hao walihojiwa na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) na kisha kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kirinyaga.

Mkuu wa Polisi wa Kirinyaga Mashariki Antony Wanjuu aliwataka wakulima kuwa na utulivu huku polisi wakiendelea kufanya uchunguzi.

“Uchunguzi umeanza na wakulima hawafai kuwa na wasiwasi kwani tumechukulia suala hili kwa uzito,” akasema.

Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, mwaka jana, aliagiza maafisa wa usalama kukabiliana na magenge ya wezi wa kawaha katika eneo la Kati.

Dkt Matiang’i aliagiza kamishna wa ukanda na kamishna wa polisi wa eneo la Kati kushirikiana na Shirika la Ujasusi nchini (NIS) kuendesha operesheni dhidi ya wezi wa kahawa.

Lakini inaonekana kuwa maafisa wa usalama wameshindwa kuangamiza wizi wa zao hilo ambalo ni kitega uchumi kikuu cha watu wa eneo la Kati.

You can share this post!

Mbunge adai Moi alitawazwa na matapeli

Pesa zaidi zitengewe matibabu ya saratani, magavana wasema

adminleo