NYS yashindwa kulipia makurutu karo ya vyuo anuwai
DAVID MUCHUI Na BENSON MATHEKA
MAKURUTU zaidi ya 16,000 wa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), wamefukuzwa katika vituo vya mafunzo anuai nchini baada ya shirika hilo kushindwa kulipa malimbikizi ya karo ya zaidi ya Sh3.3 bilioni.
Haya yanajiri wiki tatu baada ya mkurugenzi mkuu wa NYS, Matilda Sakwa kufichua kuwa linakumbwa na uhaba wa fedha na halitaweza kutekeleza baadhi ya miradi yake.
Kwa wakati huu, shirika hilo linafadhili wanafunzi 16,292 katika vyuo vya mafunzo anuai kote nchini na limechelewa kulipa karo. Kufuatia malimbikizi ya karo, wakuu wa muungano wa vyuo vya mafunzo anuai nchini (Katti) wameamua kuwafukuza wanafunzi.
Kulingana na barua ya mwenyekiti wa muungano huo, Bi Glory Mutungi kwa wakuu wa vyuo vya mafunzo anuai nchini, uamuzi huo ulifikiwa baada ya mkutano kati ya NYS na wizara ya elimu.
“Imeamuliwa kuwa wanafunzi wa NYS hawataruhusiwa kurejea vyuoni hadi NYS ilipe malimbikizi ya karo inayodaiwa na kila chuo,” inasema barua hiyo.
Akiongea na Taifa Leo, Katibu wa mafunzo anuai katika wizara ya elimu, Dkt Kevit Desai alisema vyuo hivyo vilichukua hatua hiyo kwasababu ya matatizo ya kifedha yanayotokana na hatua ya serikali ya kupunguza karo ili kuvutia wanafunzi wengi.
“Kila mwanafunzi wa NYS hulipa Sh109,500 kwa mwaka. Kwa wakati huu NYS inadaiwa na vyuo vyetu Sh3,333,068,637. Kwasababu ya deni hili, vyuo hivyo vinakabiliwa na uhaba wa pesa,” alisema Dkt Desai.
Alisema kupunguzwa kwa karo kumeongeza mzigo wa kifedha wa vyuo hivyo.
“Chuo cha ufundi cha kitaifa kinahitaji wanafunzi 10,000 kiweze kuhudumu vyema ilhali chuo cha mafunzo anuai kinahitaji wanafunzi 5,000. Bila karo, ni vigumu kuendesha shughuli zake,” alisema.
Dkt Desai alisema serikali inalenga kusajili vijana 400,000 kujiunga na vyuo vya mafunzo ya kiufundi kufikia mwaka ujao kupitia mpango wa kupunguza karo.
Mnamo Agosti 24, mwaka huu, Bi Sakwa alisema NYS imelazimika kupunguza idadi ya makurutu kutoka 30,000 hadi 20,000 baada ya bajeti yake kupunguzwa.
Alisema shirika hilo halitaweza kutekeleza baadhi ya miradi yake. “Tunapanga kupunguza idadi ya makurutu tutakaosajili mwaka huu ili kupunguza gharama na kuweka mikakati ya kuongeza mapato,” Bi Sakwa aliambia kamati ya bunge kuhusu Leba.
Alisema NYS ilikuwa imeomba Sh35 bilioni katika bajeti ya mwaka wa 2019/2020 lakini lilitengewa Sh12.7 bilioni pekee.
Kulingana na Bi Sakwa, NYS imetambua miradi ambayo itasitishwa kutokana na ukosefu wa fedha.
“Tumelazimika kusimamisha mradi wa mabasi ya uchukuzi jijini Nairobi kwa sababu hatungeuendeleza kwa sababu ya gharama,” alieleza.
Bi Sakwa aliteuliwa kusimamia shirika hilo wakati ambao lilikuwa limekumbwa na kashfa za mabilioni ya pesa.
Washukiwa kadhaa, wakiwemo wakurugenzi waliotangulia walishtakiwa kortini na kesi zinaendelea.