Habari Mseto

Gavana ataka kaunti ziwe na uhuru wa kununua dawa zao

September 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na OSCAR KAKAI

GAVANA wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Prof John Lonyangapuo ameisuta serikali kuu kuhusu sera ya kulazimu serikali za kaunti kuagiza dawa kutoka kwa shirika moja pekee.

Kulingana naye, hatua hiyo imechangia kucheleweshwa kwa dawa zinazohitajika katika hospitali za kaunti.

Prof Lonyangapuo alisema sheria kwamba Mamlaka ya Usambazaji wa Dawa Kenya (KEMSA) pekee ndiyo isambazie kaunti dawa, imepelekea vituo vingi vya afya kusubiri kwa kipindi kirefu kwani kuna mahitaji mengi yanayotakikana kutimizwa katika KEMSA kabla ya dawa kufika.

Alisema kuwa serikali inafaa kupeana kazi hiyo kwa mashirika mengine ili serikali za kaunti zinunue dawa kwa urahisi.

“Afya ni mojawapo ya ajenda kuu za serikali na haitawezakana kutimizwa ikiwa KEMSA haitoi huduma zinazotakiwa. Tunaweza kuamua kupata dawa kutoka kwa mashirika mengine kwani hatuwezi kukaa kitako na kutazama watu wetu wakiumia,” akasema Prof Lonyangapuo.

Alitoa changamoto kwa serikali kubadilisha sheria hiyo ili dawa zifike katika hospitali kwa wakati ufaao.

Gavana huyo alikuwa akiongea mjini Kapenguria alipozindua usambazaji wa dawa zinazogharimu Sh48 milioni zitakazosambazwa kwenye vituo vya afya kaunti nzima.