Habari Mseto

Wakazi wa Ngoliba waahidiwa kupata maji safi

September 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

UHABA wa maji katika eneo la Ngoliba, Thika Mashariki, katika Kaunti ya Kiambu unatarajiwa kwisha hivi karibuni.

Wakazi wa eneo hilo wanatarajia kupata maji safi kwa chini ya miezi miwili zijazo kulingana na wahandisi wanaoendesha mradi huo.

Mbunge wa Thika Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alizuru eneo hilo na kutoa hakikisho kuwa maji safi yataletwa ili wakazi wapatao 3,000 wanufaike pakubwa na mradi huo.

“Ajenda yangu muhimu ni kuona kila mwananchi wa eneo hili ananufaika na kupata maji safi yatakayosambazwa katika kila boma. Tayari maeneo muhimu ninayolenga kwa sasa ni kituo cha polisi cha Ngoliba, shule ya upili na ya msingi Ngoliba, kituo cha biashara cha eneo hilo halafu tumalizie makazi ya wananchi,” alisema Bw Wainaina.

Kulingana na wakazi wa eneo hilo linalopakana na Kaunti ya Machakos, hulazimika kutembea umbali wa kilomita kadhaa kutafuta maji safi ya kunywa.

Kiasi cha pesa

Mbunge huyo alisema mradi huo utagharimu takribani Sh30 milioni ili kuwanufaisha wakazi wote wa eneo hilo.

“Hapo awali – kama miaka tano iliyopita – serikali ilitoa Sh409 milioni za mradi wa maji wa kunufaisha eneo la Thika Mashariki lakini fedha hizo ilidaiwa zilifujwa na waliopewa jukumu la kuendesha mradi huo. Kwa wakati huu wakazi wa Ndula, Magogoni, wanapata maji safi baada ya kujengewa tanki la maji linalosambaza maji kwa zaidi ya watu 20,000,” alisema Bw Wainaina.

Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya mseto ya Ngoliba Bi Esther Kamau alisema kwa zaidi ya miaka mitano tangu kujiunga na shule hiyo wamekuwa wakitafuta maji wakitumia punda.

“Jambo hilo ni changamoto kubwa kwetu ikizingatiwa ya kwamba shule hiyo ni ya mseto. Tunatarajia mradi huo ukikamilika wanafunzi watapata afueni kwani maji yatakuwa karibu sana,” alisema Bi Kamau.

Aliwahimiza wazazi washirikiane na shule ili kukabiliana na suala la dawa za kulevya ambazo wakati mwingine zinaweza kupitishwa hadi shuleni.

Naye Bw Wambua Wakivyatu, mkazi wa eneo hilo alisema matumaini yao kwa sasa ni kuunga mkono mradi huo ili baada ya miezi mitatu hivi wawe wamepata maji safi.

“Sisi wakazi wa Ngoliba tumeumia kwa zaidi ya miaka 40 bila kupata maji safi lakini kwa sasa tunaona mwanga ukija mbele yetu,” alifafanua Bw Wakivyatu.