Makala

TAHARIRI: Siasa za 2022 haziwasaidii raia

March 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

KILA baada ya uchaguzi mkuu kukamilika na hali ya kawaida kurejelewa, viongozi wa kisiasa huanza kujadili kuhusu uchaguzi unaofuata katika muda wa miaka mitano inayokuja. Mambo sio tofauti wakati huu kufuatia kukamilika kwa uchaguzi wa mwaka 2017.

Tumeanza kusikia mijadala ya viongozi wa kisiasa kuhusu ni nani anayefaa kuchaguliwa 2022, mikakati ya kuleta makabila tofauti katika makundi yapi na ni nani ambaye hafai na mengineo.

Ni makosa makubwa kwa viongozi kuweka nchi katika hali ya uchaguzi kila mara. Hii ni kwa sababu badala ya kutekeleza ahadi ambazo walitoa nao upinzani kuhakikisha walio madarakani wanafanya kazi yao ipasavyo, fikra za Wakenya zinawekwa mawazo ya uchaguzi usio na kikomo.

Ingawa ni haki ya wanasiasa kujipanga kwani azma yao kuu ni kuwa madarakani, ni jambo la busara zaidi kuafikia haya kwa kujishughulisha zaidi na utendaji kazi unaolenga kuinua maisha ya Wakenya na kuhakikisha demokrasia na utawala bora zinazingatiwa.

Lakini tabia ya kujadili siasa za ni nani atakayechaguliwa rais 2022 asubuhi hadi jioni kana kwamba zitaboresha maisha ya Wakenya ni ya kupotosha na iliyopitwa na wakati. Hii ni tabia ya kuelekeza nchi gizani badala ya mwangani.

Siasa ambazo Wakenya wanahitaji kwa sasa ni jinsi ugawaji wa raslimali za kitaifa unavyoweza kufanywa kwa uwazi ili kusaidia kila pembe ya nchi, kumaliza ufisadi, kuboresha elimu, kuzalisha chakula zaidi, uchumi, na mambo mengine yanayohusu ustawi wa nchi.

Siasa za wakati huu pia zinafaa kushirikisha masuala ya sheria zinazostahili kufanyiwa marekebisho ili kumfaa mwananchi.

Wanasiasa wanapasa kufahamu kuwa walichaguliwa kufanyia wananchi kazi wala sio kuwasumbua kwa mijadala isiyo na maana kwao kwani wakati wake haujafika.

Mikakati yao ya 2022 inaweza kuwa na manufaa zaidi iwapo itajengwa kwenye misingi ya yale ambayo watakuwa wamefanyia wananchi kufikia wakati huo.

Kelele za kila mara kuwa huyu analenga kumaliza yule asishinde kwenye uchaguzi wa 2022 ni siasa za kupoteza wakati ambao wengi wanahitaji kuweza kutafutia familia zao riziki na kujiimarisha maishani.

Wanasiasa wanapasa kukomesha mijadala ya 2022 na badala yake waheshimu wapigaji kura kwa kutekeleza waliyoahidi.